Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (aliyesimama) akifafanua hoja za wabunge kwenye semina ya Sekta ya Uvuvi kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Katikati Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa na kushoto Katibu Mkuu Uvuvi, Dkt. Yohana Budeba.(Picha na John Mapepele)
Mbunge wa Kiteto, Mheshimiwa Emmanueli Papian akichangia hoja kwenye semina ya Sekta ya Uvuvi kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Picha na John Mapepele)
bunge wa Kyerwa mkoani Kagera, Innocent Bilakwate akichangia hoja kwenye semina ya Sekta ya Uvuvi kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Picha na John Mapepele)
Na John Mapepele, Dodoma
BUNGE limejitosa kuunga mkono vita dhidi ya uvuvi haramu iliyotangazwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kutaka viongozi wa ngazi zote wanaoshiriki au kufadhili uvuvi haramu watajwe kwa majina ili Taifa liweze kuwafahamu.
Hali hiyo itasaidia kumaliza kabisa tatizo la uvuvi haramu lililosababisha nchi ishindwe kunufaika na rasilimali hizo muhimu za uvuvi licha ya kuwa na eneo kubwa la maziwa,mito na bahari lenye jumla ya kilomita za mraba 346,337 sawa na asilimia 36.7 ya eneo lote la Tanzania ni maji.
Wakichangia mjadala katika semina kwa wabunge kuhusu vita dhidi ya uvuvi haramu iliandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kufanyika ukumbi wa Pius Msekwa bungeni jijini Dodoma baadhi ya wabunge hao waliitaka Serikali kuchukua hatua kali zaidi kwa watu wote wanaojihusisha na kufadhili uvuvi haramu ili nchi iweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu.
Mbunge wa Kyerwa mkoani Kagera, Innocent Bilakwate alisema mambo mengi katika Taifa letu kwa miaka mingi yamekuwa hayaendi kwa sababu ya viongozi waliopewa dhamana kushindwa kuchukua hatua
“Naomba Serikali iendelee kuchukua hatua kali zaidi za kupambana na uvuvi haramu na niombe waheshimiwa wabunge tushirikiane katika vita hii mambo mengi yameharibika kwa ajili ya sisi wanasiasa hivyo ni wakati wa kumuunga mkono Mhe Waziri na Mhe Rais katika kulinda rasilimali zetu za uvuvi”alisema Bilakwate.
Naye Mbunge wa Kiteto, Emmanueli Papian alisema anaamini suala la uvuvi haramu litafika mwisho na heshima ya Tanzania itarudi kutokana na maamuzi magumu yanayochukuliwa na Serikali huku akiitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutaja hadharani orodha ya viongozi wote wanaoshiriki na kufadhili uvuvi haramu ili Taifa liweze kuwafahamu kwa majina watu wanaohujumu rasilimali na kisha hatua stahiki zichukuliwe bila kujali nafasi za vyeo vyao .
Pia Mbunge huyo pia aliitaja nchi ya Uganda kama kielelezo cha mapambano dhidi ya uvuvi haramu kutokana na juhudi kubwa wanazofanya Serikali ya nchi hiyo na kuiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwachukua baadhi ya wabunge na waandishi wa habari kwenda nchini Uganda kuona namna wanavyoshughulikia uvuvi haramu.
“Kule Uganda wameweka Sheria kali ambazo zimetokomeza kabisa uvuvi haramu, naamini hili suala hili la uvuvi haramu litafika mwisho katika nchi yetu na heshima inarudi kutokana na maamuzi magumu yanayochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano ni vema tukubaliane hapa Waziri taja hadharani viongozi wanaofadhili uvuvi haramu”alisisitiza
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa, alimhakikishia Waziri Mpina kuwa Bunge linaunga mkono vita dhidi ya uvuvi haramu na kutaka orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kujihusisha au kufadhili uvuvi haramu itajwe ili Bunge liweze kuwafahamu na hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.
Awali akizungumza katika semina hiyo Waziri Mpina alisema inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 70 na 90 za nyavu zilizokuwa Ziwa Victoria zilikuwa haramu pamoja na matumizi makubwa ya sumu aina ya Theodani na Thonex, aidha katika operesheni inayoendelea maarufu kwa jina la ‘Operesheni Sangara 2018 ‘ jumla ya nyavu haramu zenye urefu wa mita milioni 34 zimekamatwa na kuteketezwa kwa moto, nyavu hizo zimekamatiwa katika maeneo mbalimbali ya ziwani,mipakani,madukani,kwenye maghala na viwandani.
“Kama zana hizi haramu zingeendelea kubaki majini shughuli za uvuvi katika ziwa Victoria zingekoma”alisema.
Alisema jumla ya kilo 310,569 za samaki zilizokuwa zimevuliwa kwa njia haramu na kinyume cha sheria zimekamatwa na kutaifishwa na Serikali kati ya samaki hao jumla ya kilo 132, 325 za samaki wachanga na wazazi zimegawiwa kwenye hospitali, shule, magereza na wananchi na pia kilo 178,244 za kayabo na kilo 4,967 za mabondo zimeuzwa kwa njia ya mnada na fedha kuingia kwenye mfuko wa Serikali.
Akielezea kuhusu ukwepaji mkubwa wa kodi za Serikali, Waziri Mpina alisema kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikipata kiasi kidogo cha mapato kutokana na biashara ya mazao ya uvuvi ambapo inakadiriwa kuwa chini ya asilimia 25 ya kiasi cha mapato inayostahili.
“Baada ya kuanza kwa operesheni mapato yatokanayo na uvuvi yaliongezeka kwa asilimia 300, katika ukanda wa Ziwa Victoria ambapo katika soko la Kirumba Mwanza kwa miezi mitatu kabla ya operesheni makusanyo yalikuwa sh. milioni 104 na baada ya kuanza operesheni makusanyo yamefikia sh. milioni 335, hii ni mara tatu ya makusanyo ya awali”alisema Mpina.
Akizungumzia utoroshaji wa mazao ya uvuvi, Waziri Mpina alisema katika mpaka wa Tanzania na Zambia ulioko Tunduma mwaka 2016/2017 jumla ya kilo 5,398,900 za dagaa zilipitishwa kwa magendo kwenda nchi za Zambia na Malawi , kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Sirari jumla ya kilo 876,500 za dagaa zilisafirishwa kwa njia za magendo na kuvushwa kwenda nchi ya Kenya. Aidha kwa mipaka hiyo pekee Serikali imepoteza jumla ya sh. bilioni 1.14 kwa kipindi hicho.
Aliongeza kuwa wakati mwingine mauzo ya Sangara nje ya nchi, Tanzania na Kenya yamekuwa ya kilingana licha ya kuwa Tanzania inamiliki asilimia 51 ya Ziwa Victoria huku Kenya ikiwa na asilimia 6 tu.
Kwa upande wake mtoa mada kuhusu Operesheni MATT, Inspekta wa Polisi, Juma Muhada alisema uvuvi haramu wa kutumia mabomu umepungua kwa asilimia 88 ambapo kabla ya Serikali kuanza kuchukua hatua hizi mabomu yalikuwa yakipigwa kila sehemu katika ukanda wa pwani ambapo wavuvi wengi walijeruhiwa na wengine kupoteza maisha.
Alisema hali hiyo ilichangia kutishia usalama ambapo pia ilisababisha baadhi ya watalii kuogopa kuja nchini mwetu ambapo inakadiriwa mlipuko wa bomu moja huathiri mzunguko wa mita 15 hadi 20 na kuua samaki na viumbe vingine vyote mayai na mazalia yake.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kusimamizi wa Bahari Kuu(DSFA) Dkt. Omary Ali Amir akitoa mada kuhusu Operesheni Jodari alisema kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikipata mapato kidogo sana kutokana na uvuvi wa ukanda wa bahari kuu(EEZ).Meli za kigeni zinazokuja kuvua nchni mauzo yao ni wastani wa shilingi bilioni 450 kwa mwaka lakini wastani wa mapato ya Serikali kwa mwaka ni bilioni 3.2 tu.
Alisema katika Operesheni inayoendelea meli 21 kati ya 24 zilizokaguliwa zilikutwa na makosa, ambapo meli 20 zilipigwa jumla ya faini ya shilingi bilioni 20 kutokana na makosa mbalimbali wakati meli moja ya Buah naga One imefikishwa katika Mahakama ya Mtwara na kesi inaendelea.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Emmanuel Bulayi akiwasilisha Mada ya Operesheni Sangara 2018 kweye ukanda wa Ziwa Victoria alisema vita dhidi ya uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi haina suluhu ambapo alisema hivi sasa kumeibuka biashara ya mabondo ambayo imechochea kasi ya uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi, bei ya kilo moja ya bondo inauzwa kati ya shilingi 70,000 hadi shilingi 900,000.Thamani ya bondo ni kubwa kuliko samaki mwenyewe.
Alisema jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 7 zimekusanywa kutokana na mauzo ya samaki, kayabo na mabondo pamoja na faini katika Operesheni hiyo.