WATAFITI WA KODI AFRIKA WAJENGEWA UWEZO

April 15, 2018
Watafiti wa Kodi Barani Afrika wameshauriwa kuimarisha mtandao wao ili kuweza kusaidiana kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika jitihada zao za kufanya utafiti.


Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Michael John wakati akifunga warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Mtandao wa Watafiti wa Kodi Afrika (ATRN) ambayo imeandaliwa na Taasisi ya Usimamizi wa Kodi Barani Afrika (ATAF) kwa kushirikiana na Chuo cha Kodi (ITA).


Bw. Michael amesema kwamba watafiti hao wanategemewa sana na mamlaka za mapato wanazoziwakilisha hivyo kuwataka kutumia ujuzi wa utafiti walioupata wakati wa mafunzo hayo ya siku nne kutatua changamoto mbalimbali na kuziongezea uwezo mamlaka za mapato barani Afrika hivyo kupelekea kuongeza makusanyo.


“Nina imani kwamba baada ya mafunzo haya mtaendelea kushirikiana kupitia mtandao wenu ili kwa pamoja mtimize lengo lenu la kutatua changamoto katika utekelezaji wa taratibu, sheria na sera za kodi barani Afrika kupitia utafiti mtakaoufanya”.Aidha amewataka watafiti hao kuzitumia vyema nyenzo za ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa ambazo wamepatiwa wakati wa mafunzo hayo ambayo yamefanyika Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi huyo wa Rasilimali Watu na Utawala ameipongeza Taasisi ya Kodi Barani Afrika pamoja na Chuo cha Kodi kwa kuandaa na kufanikisha mafunzo hayo ambayo ni muhimu katika utendaji wa usimamizi wa Kodi barani Afrika.


Naye Mkuu wa Chuo cha Kodi Pro. Isaya Jairo ameishukuru ATAF na TRA kwa kukiamini Chuo cha Kodi kuendesha mafunzo kwa watafiti ambao wametoka nchi mbalimbali za Afrika. Ambapo pia amewapongeza washiriki hao kwa kupatiwa nafasi kushiriki mafunzo hayo akisema kwamba ushiriki wao unadhihirisha utayari wa mamlaka za mapato barani Afrika kutatua changamoto zilizopo kwa kuwa na watafiti wenye weledi na ujuzi.


Awali akifungua mafunzo hayo, kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Kaimu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa Bw. Alfred Mregi alisema kwamba Usimamizi wa Kodi katika Afrika unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo watafiti wanategemewa kuzitatua ili taasisi zinazosimamia mapato Afrika ziwe rafiki kwa walipakodi na hatimaye kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani.


“Tunawategemea nyinyi kufanya utafiti wa mifumo ya kodi na kutoa suluhisho na mapendekezo kwa watunga sera na wasimamizi wa kodi”, alisema Bw. Mregi.


Warsha ya mafunzo kwa Mtandao wa Watafiti Afrika iliwashirikisha watafiti kutoka baadhi ya nchi za Afrika ambao mapendekezo yao ya utafiti yamekidhi vigezo kwa mujibu wa Taasisi ya Usimamizi wa Kodi Barani Afrika ambayo inaratibu Mtandao wa Wasimamizi wa Kodi Afrika kwa lengo la kuwajengea uwezo waafrika kufanya utafiti katika usimamizi, sheria na sera za kodi na kuwaunganisha watafiti hao na wanataaluma.


Washiriki wa warsha hii ambayo ni ya Tatu kufanyika, wameishukuru ATAF na Chuo cha Kodi kwa kuendesha mafunzo hayo wakisema kwamba imewapa uelewa zaidi wa kuendelea na utafiti wao.


Mafunzo hayo ambayo yaliendeshwa kwa lugha tatu: Kireno, Kifaransa na Kiingereza yaliwashirikisha washiriki 24 kutoka, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Niger, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Togo, Benin, Cape Verde, Tunisia, Ivory Coast, Kenya na Tanzania.


Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Michael John akimkabidhi mshiriki kutoka Tunisia Bw. Jabali Belhanssen cheti cha ushiriki wa mafunzo ya utafiti ambayo yafanyika jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano wa Taasisi ya Usimamizi wa Kodi Afrika (ATAF) na Chuo cha Kodi (IAT). Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo, Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma na Utafiti Dr. Lewis Ishemoi na Mwakilishi ATAF Bw. Eugenio Bras.

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Michael John (katikati) akifuatilia matukio wakati wa kufunga na kukabidhi vyeti kwa washiriki wa warsha ya mafunzo kwa Mtandao wa Watafiti wa Kodi Afrika (ATRN) ambayo imefanyika jijini Dar es salaam. Wengina kutoka kushoto ni; Mkufunzi wa mafunzo hayo Prof. Nicaise Mede kutoka Benin, Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo, Naibu Mkuu wa Chuo cha Kodi Taaluma na Utafiti Dr. Lewis Ishemoi na Mwakilishi wa Taasisi ya Utafiti Barani Afrika (ATAF) Bw. Eugenio Bras.

Baadhi ya washiriki wa Warsha ya Mafunzo kwa Mtandao wa Watafiti wa Kodi Afrika (ATRN) waliosimama wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Michael John (aliyekaa katikati) baada ya kufunga mafunzo hayo. Wengine kutoka kulia ni, Mwakilishi wa Taasisi ya Utafiti Barani Afrika (ATAF) Bw. Eugenio Bras, Naibu Mkuu wa Chuo cha Kodi Taaluma na Utafiti Dr. Lewis Ishemoi, Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo na Mkufunzi wa mafunzo hayo Prof. Nicaise Mede kutoka Benin

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »