TANZANIA YAKARIBISHA UWEKEZAJI VITUO VYA KUJAZA GESI VIJIJINI

January 25, 2025


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amesema Tanzania inakaribisha uwekezaji kutoka Uingereza kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kujaza gesi, hasa vijijini ili kuboresha upatikanaji wa gesi kwa matumizi ya kupikia kwa gharama nafuu na kwa wakati, hivyo kuchangia katika kuboresha maisha ya wananchi.

Mhe. Dkt. Biteko amesema hayo Januari 24, 2025, jijini Dar es Salaam alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young, katika mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa sekta ya nishati kati ya nchi hizo mbili. Alipongeza jitihada za Uingereza kusaidia juhudi za Tanzania katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi, hasa vijijini.

Kwa upande wake, Balozi Marianne Young ametoa pongezi kwa Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Afrika wa Nishati na kutaja kwamba hii ni hatua muhimu inayothibitisha uongozi thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha upatikanaji wa nishati safi barani Afrika. Aliongeza kuwa Uingereza itaendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia mashuleni na vijijini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »