Na Mwandishi Wetu MoHA-Dodoma
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza jukumu lake la kikatiba kwa kusimamia usalama katika mikutano na shughuli za Vyama vya Siasa bila kujali itikadi ya Chama cha Siasa chochote.
Amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kusimamia ulinzi na usalama kwa Vyama vyote vya Siasa kwa weledi katika Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mpinduzi uliofanyika Dodoma pamoja na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo uliofanyika jijini Dar es salaam.
Bashungwa ameyasema hayo leo tarehe 22 Januari 2025 wakati alipofanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dodoma ambapo amesisitiza Vyama vya Siasa kutimiza wajibu wa kutii sheria bila shuruti ili kuepuka kulazimishwa kutii sheria.
“Matarajio yangu kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ni kwamba haki hii mnayoitenda Jeshi la Polisi kwa kutoangalia itikadi, pia Vyama vya Siasa vya Upinzani na Vyama vya siasa kwa ujumla, haki hii ije na wajibu kwa wao kutii sheria bila shuruti, hakuna haki bila wajibu” amesisitiza Bashungwa
Aidha, Bashungwa ameliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kujipanga kusimamia kikamilifu usalama kwa raia na mali zao wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Waheshimiwa Madiwani, Wabunge na Rais utakaofanyika Mwaka huu 2025 ili kuendelea kudumisha usalama, amani na utulivu wa nchi yetu.
Awali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP. Camillus Wambura ameeleza kuwa Jeshi la Polisi limejiimarisha vyema kwa kuweka mikakati dhabiti ya kuimarisha usalama kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.
EmoticonEmoticon