Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Ndugu Paul Makonda atakua mgeni rasmi wa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakaowakutanisha Simba na Yanga utakaochezwa Jumapili Aprili 29,2018 Uwanja wa Taifa Dar Es Salaam.
Ndugu Makonda atawaongoza maelfu ya mashabiki wa mpira wa miguu watakaojitokeza kweye Uwanja wa Taifa kushuhudia mchezo huo namba 178 utakaoanza saa 10 jioni.
Tayari tiketi za mchezo huo zinaendelea kuuzwa ambapo VIP A ni shilingi 30,000,VIP B na C 20,000 na Mzunguko(Jukwaa la rangi ya Chungwa,Kijani na Bluu) 7,000.
Tiketi zinapatikana kupitia Selcom.
Katika mchezo huo Simba wanaingia uwanjani wakiwa wanaongoza ligi baada ya kujikusanyia pointi 59 ikicheza michezo 25 wakati Yanga wana pointi 48 wakiwa nafasi ya pili baada ya kucheza michezo 23.
VIJANA WAWILI WA KITANZANIA KUPELEKWA RUSSIA
Taasisi ya Lengo Football Academy yenye makazi yake Mkoani Arusha nchini Tanzania na Australia imeteua vijana wawili wa Tanzania wenye umri wa miaka 12 Laigwanani Lomayani Mollel na Ziporah Mollel katika mpango wake unaofahamika kama Football For Friendship.
Mpango huo wa Football For Friendship(F4F2018) umelenga katika vijana wadogo kuwa promoti,kuwakuza na kuwajenga katika kuupenda mpira.
Mpango huo wa F4F2018 umelenga kwenye kupata mchezaji mmoja na mwandishi mmoja wote wakiwa ni vijana wenye umri wa miaka 12.
Laigwanani ambaye ni mchezaji na Ziporah ambaye ni Mwandishi watapelekwa nchini Russia wakati wa Fainali za Kombe la dunia zitakazofanyika mwaka huu nchini humo wakiambatana na watu wazima wawili watakaokuwa wakiwaangalia.
Wakiwa Russia watapata nafasi ya kucheza mechi mbalimbali na wenzao kutoka nchi tofauti huku pia wakipata nafasi ya kushuhudia mechi kadhaa za kombe la dunia.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF