Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais Mh. Kangi Lugola akisalimiana na Uongozi wa Mamlaka ya maji Safi na
usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) alipofanya ziara ya kutembelea
Ofisi hizo mjini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais Mh. Kangi Lugola akifafanua jambo alipokua akiongea na Wafanyakazi
wa Mamlaka ya maji Safi na usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA)
mjini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais Mh. Kangi Lugola akielekeza jambo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Mamlaka ya maji Safi na usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) David
Palangyo wakati wa ziara ya kutembelea mabwawa ya kuhifadhi maji taka
yanayotumiwa na DUWASA katika eneo la Swaswa mjini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais Mh. Kangi Lugola akiwa pamoja na Ujumbe toka DUWASA akikagua
mabwawa ya kuhifadhi maji taka katika eneo la Swaswa na Ilazo mjini
Dodoma ambapo alifanya ziara.
Sehemu ya mabwawa ya kuhifadhia
maji taka inayotumiwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira
mjini Dodoma (DUWASA) katika eneno la Swaswa.
………………………………………………………………………….
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Kangi Lugola hii leo amefanya ziara ya
kushtukiza katika Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini
Dodoma (DUWASA) ikiwa ni pamoja na kutembelea miundombinu ya Mamlamka
hiyo.
Waziri Lugola amesikitishwa na
namna Mamlaka hiyo ilivyoshindwa kuhimili kiasi cha maji taka
yanayozalishwa katika Mji huo wa Dodoma na kutitiririka katika makazi
ya watu bila kutibiwa (Treated).
Katika ziara hiyo Naibu Waziri
Kangi Lugola ameitaka Mamlaka hiyo kuja na mpango wa haraka wa kudhibiti
maji hayo kwa lengo la kudhibiti usafi wa Mazingira na Ustawi wa
Wananchi. “DUWASA mmekuwa mkitiririsha maji taka bila kuyatibu kwenye
makazi ya watu, na kwenye kilimo cha mpunga, na mmepelekea baadhi ya
watu kuyahama makazi yao.” Lugola alisisitiza.
Aidha Waziri Lugola ameitaka
DUWASA kuhakikisha mabwawa mawili yaliyotelekezwa eneo la Swaswa
yanakarabatiwa ili kuhimili kiwango cha uharibifu wa mazingira kabla ya
tarehe 31/12/2018, na kuwataka kuimarisha ulinzi kuzunguka mabwawa yote
ili watu wasichepushe maji katika mashamba yaliyopo pembezoni mwa
mabwawa hayo.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Lugola ameitaka Mamlaka hiyo ya DUWASA kutumia gari ya matangazo
na kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa kutoa elimu kwa
wananchi wa maeneo hayo juu ya athari ya matumizi ya maji hayo machafu
DUWASA pia imetakiwa kupata
kibali kutoka kwa Mamlaka ya Bonde la Maji ya Wami-Ruvu cha kutiririsha
maji taka kwenye mazingira na kuhakikisha maji hayo yanatibiwa kwa
kiwango kinachoruhusiwa kwa mujibu wa sheria na kufanya Tathmini ya
Kimkakati ya Mazingira kuendana na ongezeko la watu.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA
Bw. David Pallangyo amesema kuwa walipokea mabwawa hayo kutoka kwa
iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) mwaka 2002 na kukiri
kutiririsha maji hayo bila kuyatibu katika mazingira.
Bw. Palangyo amebainisha kuwa
Ofisi yake ina mkakati wa muda mrefu wa kujenga mabwawa makubwa zaidi
eneo la Nzuguni ili kukidhi mahitaji ya sasa na kuendana na ongezeko la
idadi ya watu baada ya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi.