Mkuu wa wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani ,Assumpter Mshama ,aliyesimama akizungumza jambo kuhusiana na masuala ya Elimu bure .
Picha na Mwamvua Mwinyi
……………….
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha,Mkoani
Pwani, Assumpter Mshama ameamuru walimu wawili wa shule za msingi
washushwe vyeo kutoka nafasi ya mwalimu mkuu na kuwa walimu wa kawaida
,kutokana na kosa la kuchangisha michango wazazi.
Hatua hiyo ,ameichukua siku chache
baada ya mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,kukemea tabia
inayofanywa na baadhi ya walimu wakuu na bodi za shule kuchangisha
wazazi na walezi michango ambayo serikali imeizuia.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake mjini Kibaha ,alisema walimu hao wamekiuka agizo la
serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk .John Magufuli .
Mshama aliwataja walimu hao kuwa
ni mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Miembesaba, Rashinde Kilakala ambaye
alikuwa akipokea sh.1,000 kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya mitihani
jambo ambalo ni kinyume cha agizo la serikali.
Mwalimu mwingine ni wa shule ya
msingi Jitegemee, Sapiensia Kilongozi ambae aliweka kikao na kuita
wazazi na kuwataka wazazi wenye watoto watoe shilingi 2,000 kwa wiki kwa
ajili ya masomo ya ziada na mitihani.
Mshama alisema,huo ni mwanzo kwani
ataendelea kusimamia maagizo yanayotolewa na serikali ili iwe fundisho
kwa walimu wanaokaidi mipango ya serikali hiyo.
Alieleza atakaeendelea kufanya hivyo akibainika atachukuliwa hatua kali ikiwemo kufukuzwa kazi .
“Nilipata malalamiko kutoka kwa
wazazi kwamba kuna walimu wakuu wa shule hizo wanachangisha wazazi fedha
kwa ajili ya michango mbalimbali ambayo imekatazwa na siku chache
zilizopita” alisema Mshama.
“Mwalimu huyu wa shule ya
Miembesaba hana kibali wala hajapeleka barua na hakuwa na sababu wala
kibali cha kufanya hivyo ambapo mtihani wa mwisho wa mwaka kila mtoto
hutoa 1,000 na alikuwa hatoi risiti,”
“Lazima tumheshimu Rais kwani juzi
tu kaongelea suala la elimu bure,hata kama umechangisha risiti ulitoa
hivyo mpumzike nafasi hizo mbaki walimu wakawaida,” alisema Mshama.
Aidha anashangaa walimu hao walipata wapi nguvu ya kuwashawishi wazazi na kupokea fedha hizo wakati Rais alishazuia mambo hayo.
Nae mkurugenzi wa Halmashauri ya
Mji wa Kibaha ,Jeniffer Omollo alisema suala la kuchangisha michango
mashuleni lilipigwa marufuku na walimu waliaambiwa kuwa hawaruhusiwi
kuwachangisha wazazi .
Alisema kuanzia sasa watawachukulia hatua kwa mujibu wa kanuni na sheria.
Kwa upande wake mwalimu Kilakala
alisema anashindwa kueleza kwani walikubaliana na wazazi lakini
wakamgeuka kuwa walikuwa wakichanga kinyume cha taratibu hata hivyo
hawezi kusema zaidi.
Mwalimu wa shule ya msingi
Jitegemee Sapiensia Kilongozi yeye alijieleza”:niliitisha kikao cha
wazazi na kujadili masuala ya taaluma na wazazi wenyewe waliingiza
kipengele wanahitaji watoto wao wasaidiwe kwenye masomo ya ziada na
mitihani,” alisema Kilongozi.
Alisema walikubaliana baada ya
hapo wakaandika muhutasari lakini baadhi ya wazazi walikuja huku kueleza
lakini nia na madhumuni ilikuwa ni kufuata taratibu kwani asingeweza
kutoa maamuzi ya kupitisha jambo hilo ,maamuzi lazima yapelekwe kwa
ofisa elimu kata na baadaye kwa mkurugenzi.
Kutokana na hali hiyo ,Mshama alisema ni lazima wapate fundisho kwa kushushwa nafasi zao za kazi ili wabaki walimu wa kawaida.