Muimbaji nguli wa muziki wa dance, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya
pamoja na mwanae, Papii Kocha wameanza maandalizi ya ujio wao mpya, ikiwa ni
takriban miaka 14 tangu waachie kibao kipya.
Wawili hao walipewa msamaha na Rais Dkt John Magufuli kwenye
maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru. Serikali imeonesha nia ya kuwasaidia waimbaji
hao wanaopendwa sana kurejea tena kwenye muziki kwa kishindo.
Naibu Waziri wa Habari,
Sanaa, Utamaduni na Michezo, Bi. Juliana Shonza aliwakutanisha na uongozi wa
Wanene Studios waliokubali kuchukua jukumu la kuwarudisha tena kwenye muziki. Tayari
wameanza kuingia studio kuandaa kazi mpya katika studio hizo kubwa na bora
zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Wameanza kwa kufanya
photoshoot, kitu ambacho wamekiri kuwa ni kigeni mno kwao kutokana na kuwa
gerezani kwa miaka 14 na wametoka katika nyakati ambazo muziki wa Tanzania
umepiga hatua kubwa ukilinganisha na zamani.
“Miaka 14 si mchezo, mambo
kama haya si unayaona mwenyewe, niliyamiss, nimemiss vitu vingi, picha za
ukweli, mambo haya kule tulipotoka hamna. Lazima uelewe hii ni dunia
nyingine,” alisema Papii Kocha wakati wa photoshoot.
Kwa kujiamini, Papii amesema kuwa kazi zao mpya zitakuwa kali zaidi ya
zile za zamani. “Kwasababu tumejipanga vizuri na kazi zinazokuja zitakuwa nzuri zaidi
ya zile tulizofanya mwanzo,” amesisitiza Papii.
Kwenye photoshoot hiyo iliyofanywa na mpiga picha mahiri Eric Luga,
Babu Seya na Papii Kocha walivalishwa na mbunifu wa mavazi, Mtani Nyamakababi.
Unaweza kufuatilia kila hatua ya safari yao kuelekea kuachia kazi mpya
kwa kulike ukurasa wao rasmi wa Instagram @babanamwana, Facebook: baba na
mwana. Pia subscribe kwenye channel yao ya Youtube iitwayo Baba na Mwana kuona
video mbalimbali za behind the scenes.
Unaweza kuangalia video ya behind the scenes ya upigaji picha kwa
kufuata link hii >> https://youtu.be/h-Kdp87now4