Benny Mwaipaja-WFM, Dar es Salaam
Wizara
ya Fedha na Mipango Fungu Hamsini (Vote 50)linalohusika na masuala ya
utawala, limeibuka kinara kwa kupata tuzo ya mshindi wa kwanza katika
utoaji wa Taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 katika kundi la Wizara na
Idara za Serikali inayoandaliwa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu
(NBAA).
Tuzo
hizo zimetolewa kwa washindi na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Francis
Mwakapalila kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw.
Doto James katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kilichopo
Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa
Mkutano wa mwaka wa Wahasibu nchini uliofanyika katika eneo hilo.
CPA.
Mwakapalila alisema kuwa taarifa bora za fedha ni muhimu sana katika
maendeleo ya nchi kwa kuwa walipa kodi, wawekezaji na wadau wengine
hutegemea taarifa hizo katika kufanya maamuzi.
‘Kama
taarifa za fedha hazitatolewa kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati mwafaka
kunaweza kusababisha athari katika uthabiti wa mifumo ya kifedha
nchini’, alieleza CPA. Mwakapalila
Aidha
Mwakapalila amewapongeza wahasibu kwa kuamua kukaa pamoja na kujadili
taaluma ya uhasibu katika maendeleo ya viwanda ambayo ni ajenda ya
kipaumbele kwa Serikali ya awamu ya tano.
Amesema
suala la Uchumi wa viwanda ni muhimu katika kuongeza kipato na kupata
fedha za kigeni kwa njia ya kuuza bidhaa nje na pia kupata mapato ya
kodi na yasiyo ya kodi hivyo akatoa rai kwa wananchi kuendelea kujadili
masuala ya uchumi wa viwanda na kupata namna sahihi ya kuufikia ili
ndoto ya uchumi huo ziweze kuwa za kweli.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu
(NBAA), CPA. Pius Maneno amesema kuwa tuzo zinazotolewa na NBAA
zinalengo la kuhamasisha uwajibikaji na kuandaa taarifa ya fedha zilizo
na viwango vya kimataifa.
Amesema
kuwa washindi wa tuzo hizo wanapatikana kupitia mchakato uliosheheni
weledi wa hali ya juu kutoka kwa wabobezi wa taaluma ya uhasibu nchini
ambao wanaangalia vigezo kadhaa vikiwemo kuwa na hati safi na
kuwasilisha Hesabu kwa wakati na pia kufikisha kiwango cha ubora wa
taarifa kuanzia asilimia 75.
Mhasibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50, Bw. Christopher Nkupama,
amesema kuwa tuzo hiyo inawapa morali ya kufanyakazi kwa umahili zaidi
na kuwapongeza watumishi walioko katika idara yake kwa kufanyakazi kubwa
na bila kuchoka kuhakikisha kuwa wanazingatia kanuni na taratibu za
uhasibu wanapotekeleza majukumu yao.
Mshindi
wa Jumla katika tuzo hizo kwa taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 ni
Twiga Cement Plc na kwa upande wa Wizara na Idara za Serikali ni Wizara
ya Fedha na Mipango fungu hamsini (V. 50), tuzo ambayo ilipokelewa na
Mhasibu Mkuu wa fungu hilo Bw. Christopher Nkupama, ikifuatiwa na Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji fungu arobaini na nne (V.44) na Ofisi
ya Waziri Mkuu fungu ishirini na tano (V. 25)
Washiriki
wa Tuzo hizo ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wakala wa Serikali,
Wizara na Idara za Serikali na Sekta Binafsi ambapo kwa mwaka huu
waliojitokeza kutoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa walikua sita na Wizara
na Idara za Serikali walikua sita.
Jumla
ya washidani waliojitokeza ni 56 na waliofanikiwa kuvuka kigezo cha kuwa
na zaidi ya asilimia 75 walikua washidi 36 na hao walifanikiwa kushika
nafasi ya kwanza hadi ya tatu kulingana na makundi.
Vilevile
Idadi ya Wahasibu ambao wamehudhuria katika Mkutano wa mwaka ambao
hufanyika kila mwaka kabla ya kutolewa tuzo hizo imepanda kwa asilimia
60 ambapo mwaka 2016 walihudhuria wajumbe 1700 ilihali mwaka huu 2017
wamehudhuria zaidi ya wajumbe 2700.
Wahasibu
wa Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50 wakiwa katika picha ya pamoja na
Mhasibu Mkuu wa Fungu hilo Bw. Christopher Nkupama (wa pili kushoto)
baada ya kupokea Tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016
zilizotolewa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) eneo la
Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam .
Mhasibu
Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila (wa kwanza kulia) akiwa
katika picha ya pamoja na Wahasibu wa Wizara hiyo fungu 50 baada ya
kuwakabidhi tuzo hiyo katika eneo la Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam, aliyeshika tuzo ni Mhasibu Mkuu wa Fungu hilo Bw. Christopher
Nkupama.
Washindi
wa Kwanza wa makundi mbalimbali ya Tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa
mwaka 2016 zinazotolewa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA)
wakiwa katika picha ya pamoja na Meza kuu baada ya kukabidhiwa tuzo hizo
eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mmoja
wa wahasibu walioambatana na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango-fungu 50, Bw. Christopher Nkupama (hayupo pichani) akisalimiana
na meza kuu baada ya kupokea tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka
2016 iliyotolewa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) eneo la
Bunju nje kidogo ya Jiji l Dar es Salaam.
Mhasibu
Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila (wa kwanza kulia)
akimklabidhi Mhasibu wa Wizara ya Fedha na Mipango-fungu 50 (Vote 50),
Bw. Christopher Nkupama (kushoto) tuzo kwa kuwa mshindi wa kwanza wa
taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 kwa kundi la Wizara na Idara za
Serikali iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu
(NBAA) eneo la Bunju, Nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wa pili kulia
ni Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA. Pius Maneno.
Mhasibu
Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila akieleza kuwa Uhasibu ni
taaluma muhimu katika maendeleo ya Viwanda kwa kuwa wawekezaji hutumia
taarifa za fedha zinazoandaliwa ili kutoa maamuzi, wakati wa kuhitimisha
mkutano wa mwaka wa Wahasibu na kugawa tuzo ya taarifa bora ya fedha
kwa washindi wa mwaka 2016, katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi eneo la
Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mhasibu
Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila (kushoto) akizungumza jambo
na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu
(NBAA) CPA. Pius Maneno muda mfupi kabla ya kutoa tuzo za taarifa bora
ya fedha kwa mwaka 2016 katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu
kilichopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango