Profesa Joyce Ndalichako Waziri
wa Elimu Sayansi na Teknolojia akiwa na viongozi wa Mkoa wa Geita wakati
wa kukagua vyumba vya madarasa mwenye miwani kulia ni Mhandisi Robert
Gabriel Mkuu wa Mkoa Geita.
Jengo la bwalo la wanafunzi wa
Shule ya Sekondari Magufuli lililopo Kata ya Bwanga Wilayani Chato
ambalo limejengwa kupitia mpango wa lipa kulingana na matokeo (P4R).
Moja ya bweni la wanafunzi Shule ya Sekondari Magufuli lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 80 ambalo limetekelezwa kupitia P4R.
Profesa Joyce Ndalichako Waziri
wa Elimu Sayansi na Teknolojia akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa
shule ya sekondari Magufuli, wakwanza kulia ni Mkuu wa shule hiyo na
wapili kulia ni Shaban Ntarambe Mkuu wa Wilaya Chato.
Mheshimiwa Shaban Ntarambe Mkuu
wa Wilaya ya Chato akizungumza na wananchi (awapo kwenye picha) wakati
wa ziara ya Waziri wa Elimu Wilayani Chato.
Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi
Mkuu wa Mkoa wa Geita akizungumza jambo wakati wa ziara ya Waziri wa
Elimu Sayansi na Teknolojia Magufuli Sekondari.
Waziri wa Elimu Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wananchi wa kijiji
cha Bwanga wakati wa Ziara yake Magufuli Sekondari.
Bwana Exvery Nkanga kaimu Afisa
Elimu Mkoa wa Geita akisoma taarifa ya maendeleo ya elimu Mkoa wa Geita
kwa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia.
…………………………………………………………………………………………………
Na: Magesa Jumapili-Afisa Habari- Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Waziri wa Elimu Sayansi na
Teknolojia Pro.Joyce Ndalichako amefanya ziara fupi Wilayani Chato kwa
kuitembelea Shule ya Sekondari Magufuli na kukagua utekelezaji wa miradi
ya lipa kulingana na matokeo(P4R) shuleni hapo.
Akizungumza baada ya kufanya
ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa mabweni, Bwalo, vyoo na vyumba vya
madarasa Profesa Joyce Ndalichako ameupongeza Uongozi wa Mkoa,
Halmashauri ya Chato na Shule ya Sekondari Magufuli kwa kusimamia vizuri
fedha za utekelezaji wa miradi hiyo kwa ubora na kiwango kinachotakiwa.”Nafurahi
kuona fedha za P4R zinatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa kama
tulivyokagua na kujionea kiwango kilichojengwa ndio haswa kinachotakiwa
ambacho darasa lazima liwe na silling bodi, umeme lakini pia liwe na
madirisha tofauti na madarasa tuliyokuwa tunajenga zamani hivyo
nawapongeza kwa dhati kabisa viongozi mmefanya kazi kubwa thamani ya
fedha inaonekana”.
Profesa Ndalichako amesema
Serikali ya awamu ya tano inajukumu kubwa la kuhakikisha kunakuwa na
mazingira bora katika utoaji wa elimu hivyo miradi ya namna hii
inatekelezwa katika Halmashauri nchi nzima. Amesema mwezi desemba 2017
serikali imetoa kwa halmashauri zote shilingi bilioni 15 na milioni 900
za kuendeleza jitihda za kuimarisha miundombinu ya sekta ya elimu ili
kuongeza na kuimarisha majengo kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa darasa
la kwanza ambapo zitajenga jumla ya madarasa 415, mabweni 46, matundu ya
vyoo 814 na mabwalo 7.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Geita
Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi amempongeza Waziri wa elimu kwa
kutembelea shule hiyo ili kujionea kazi nzuri iliyofanyika licha ya
kuwa na majukumu mengi ya kitaifa. Amewashukuru wananchi wa Mkoa wa
Geita kwa jitihada zao za kushiriki katika ujenzi wa nyumba vya madarasa
8000 kwa shule za msingi na Sekondari ambapo tangu mkoa uzindue
kampeni ya ujenzi huo zaidi ya vyumba 900 vya shule za msingi na zaidi
ya 130 vya Sekondari vipo katika hatua tofauti. Amesisitiza kuendelea
kuunga mkono jitihada zao kwa kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika
michango inayotolewa na wananchi.
Mhandisi Robert Gabriel
amemhakikishia Waziri wa Elimu kuwa pamoja na kuwa na idadi kubwa ya
wanafunzi walioandikishwa kujiunda na elimu ya awali, darasa la kwanza
na Sekondari hakutakuwa na mwanafunzi atakaye kaa nje ya darasa kwa kuwa
jitihada za zinafanyika kwa haraka ili kukabiliana na hali hiyo.
Akiwa katika shule hiyo
Mheshimiwa Waziri wa elimu alikagua ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa,
matundu 20 ya vyoo, mabweni 2 ya kulala wanafunzi na bwalo miradi yote
hii imetekelezwa na Serikali kupitia mpango wa lipa kulingana na matokeo
kwa gharama ya shilingi 570,500,000/=.