Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.
Mchezaji
wa timu ya Singida United ya Singida, Mudathir Yahaya amechaguliwa kuwa
Mchezaji Bora wa Mwezi Novemba, 2017 wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.
Mudathir alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Beki
Asante Kwasi wa Lipuli ya Iringa na Mshambuliaji Danny Usengimana pia wa
Singida United, alioingia nao fainali ya kuwania nafasi hiyo.
Katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii kwenye kikao cha
Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo
viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida United mwezi huo
ikipata pointi saba katika michezo mitatu iliyocheza na kupanda katika
msimamo wa ligi kutoka nafasi ya sita iliyokuwepo mwezi Oktoba hadi ya
nne.
Singida United ilitoka 0-0 na Yanga, iliifunga Mbeya City mabao 2-1
na pia iliifunga Lipuli bao 1-0, ambapo Mudathir anayecheza nafasi ya
kiungo alicheza dakika zote 270 sawa na michezo mitatu na hakuwa na kadi
yoyote.
Alitajwa mchezaji bora wa mchezo wa Singida United na Yanga
uliofanyika Uwanja wa Namfua, Singida, alicheza kwa kiwango cha juu
wakati Singida United ilipochuana na Lipuli, pia alisaidia kutengeneza
nafasi ambazo zilitumiwa vyema na wenzake katika kupata ushindi dhidi ya
Mbeya City, huku yeye akihusika kwa kwa kiasi kikubwa kupambania
ushindi huo.
Mafanikio yake kwa mwezi huo yalisaidia kumrudisha katika kikosi cha
timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na kile cha Zanzibar ‘Zanzibar
Heroes’, ambacho kinashiriki michuano ya Chalenji inayoendelea nchini
Kenya.
Kampuni ya Vodacom, ambao ndiyo wadhamini wa ligi hiyo ina utaratibu
wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu
kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka
2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali.
Mudathir atazawadiwa Sh milioni moja kutoka Vodacom pamoja na kisimbusi (decoder) cha Azam kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.