Na Lilian Lundo na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli amesamehe jumla ya wafungwa 8,157 katika
maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika leo
katika uwanja wa Jamhuri, Mjini Dodoma.
Msamaha
huo umehusisha wafungwa 1828 ambao watatolewa kaunzia leo na wengine
6329 wamepunguziwa muda wa vifungo vyao, aidha kati ya wafungwa
watakaoachiwa huru wafungwa 61 ni wafungwa ambao walihukumiwa kunyongwa.
“Kuna
wafungwa ambao wamehukumiwa kunyongwa wana umri wa miaka 85 na wapo
waliokaa gerezani zaidi miaka ya miaka 45, ambao wametubu na kukiri
makosa na wapo ambao hawakuwauwa maalbino wala hawakuwa majambazi,”
amesema Dkt. Magufuli.
Dkt.
Magufuli ametoa mfano wa mfungwa anayejulikana kama Mganga Matonya
mwenye umri wa miaka 85 yupo kwenye orodha ya wafungwa watakaoachiwa
huru leo ambapo amekaa gerezani kwa miaka 37 na mahabusu miaka saba (7)
kabla hajahukumiwa.
Katika
hatua hiyo, Rais Dkt. Magufuli amewaachia huru Nguza Viking na Johson
Nguza (Papii Kocha) waliohukumiwa kifungo cha maisha.
Aidha
Mhe. Rais amesema kuwa msamaha huo alioutoa leo umetokana na mamlaka
aliyonayo kutoka kwenye Ibara ya 45 (a) (b) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayomruhusu Mhe. Rais kutoa msamaha, kumuachia
huru, kubadilisha adhabu au kufuta adhabu kwa mtu yoyote aliyehukumiwa
kwa kosa lolote.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa wito kwa watanzania wote kuenzi na kudumisha tunu na amani zilizoachwa na waasisi wa Taifa.
Aidha,
Rais Magufuli ameeleza kuwa tangu nchi ipate uhuru kumekuwa na
maendeleo katika nyanza mbalimbali ikiwemo barabara, madaraja, vituo vya
afya, shule za msingi na shule za sekondari.
“Wakati
nchi inapata uhuru kulikuwa na jumla ya kilometa 32,600 za barabara
ambapo kilometa 1360 zilikuwa katika kiwango cha lami, lakini mpaka sasa
nchi inapotimiza miaka 56 ya uhuru kuna jumla ya kilometa 122,500 za
barabara ambapo kati ya hizo kilometa 12,679.55 zipo katika kiwango cha
lami, kilometa 2,480 zinaendelea kujengwa katika kiwango cha lami na
kilometa 7087 zipo kwenye hatua mbalimbali za maandalizi za kujengwa
katika kiwango cha lami” anasema Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli amesema kuwa, Mfalme wa Morroco amemtuma Spika wa nchi
hiyo kuja kuangalia eneo litakalojengwa uwanja mkubwa wa Kimataifa Mkoa
wa Dodoma ambapo unatarajiwa kuwekwa jiwe la msingi mwezi Machi au
Aprili mwaka 2018.
Mbali
na hayo Sherehe hizo zilipambwa na gwaride kutoka Majeshi ya Tanzania,
onesho la kikundi cha Komando, onesho la gwaride la Uzalendo la
wanafunzi, vikundi mbalimbali vya kwaya, ngoma za alisi na Tanzania
Allstars.