Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.
Kocha
Mkuu wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje amepanga
kesho Jumanne Desemba 5, 2017 kuanza kufanyia kazi upungufu ulioonekana
kwenye mchezo dhidi ya Libya uliofanyika Jumapili Desemba 3, mwaka huu.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kenyatta ulioko Machakos hapa
nchini Kenya, Tanzania Bara ilipata sare katika safari ya kuwania Kombe
la Cecafa – michuano inayofanyika hapa Kenya.
Ninje amesema katika mchezo huo wa kwanza waliecheza katika kiwango
cha kuridhisha na kikubwa anataka kuangalia namna ya kufanyia kazi
upungufu ikiwa ni pamoja na pale timu inapopoteza mpira.
Anasema kwenye mchezo dhidi ya Libya timu ilicheza kuanzia nyuma
kupitia sehemu ya kiungo na kuunganisha sehemu ya ushambuliaji – jambo
ambalo limemfurahisha kwa namna timu ilivyotengeneza nafasi.
Akizungumzia mchezo unaofuata dhidi ya Zanzibar Heroes, Ninje amesema
ni mchezo mgumu kama ambavyo historia inaonesha wakati timu hizo mbili
zinapokutana.
“Lakini kuanzia mazoezi ya kesho nitaiandaa timu kupata ushindi na
nimepanga kwenda kuitazama Zanzibar itakapocheza mchezo wake wa kesho
dhidi ya Rwanda,” amesema.
Amesema ataiangalia Zanzibar Heroes kiufundi ili kubaini upungufu wao
ili naye ajue namna atakavyoweza kutumia nafasi hizo kwenye mchezo
unaofuata.
“Ni fahari kwa timu zetu hizi mbili kila mmoja kupambana kupata
pointi bahati nzuri wao wanacheza kesho kwa hiyo mchezo wao nitautumia
kutazama mapungufu (upungufu wao) yao yatakayoweza kutusaidia,’’ alisema
Ninje.
Leo Desemba 4, mwaka huu asubuhi kikosi cha Kilimanjaro Stars
kimefanya mazoezi ya kuondoa uchovu baada ya mechi ya jana kabla ya hapo
kesho kuanza rasmi kujiandaa kwa mchezo huo unaofuata.
Mbarak Yusuph ndiye mchezaji pekee ambaye hakufanya mazoezi hayo baada ya kuumia misuli kwenye mchezo wa jana dhidi ya Libya.
Mbarak atapumzishwa kwenye mchezo unaofuata ili kuwa tayari kuikabili Rwanda.
Leo jioni Kocha Ninje atakutana na wachezaji kuutathmini mchezo wa
Libya ambao ulimalizika kwa sare ya bila kwenye Uwanja wa Kenyatta,
Machakos.
Kilimanjaro Stars ipo kundi A pamoja na timu za Zanzibar, Libya, Rwanda na wenyeji Kenya.
Kenya wana pointi tatu baada ya kuifunga Rwanda mabao 2-0 wakati
Kilimanjaro Stars na Libya wana pointi 1 kila mmoja baada ya kutoka sare
ya bila kufungana kwenye mchezo wao wa kwanza wakati Zanzibar na Rwanda
wenyewe hawana pointi huku Zanzibar ikiwa haijashuka dimbani katika
kundi hilo.