Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akioneshwa ramani ya Hifadhi ya
Taifa ya Saadani na Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Vitalis
Kuluka huku akishirikiana kuonesha eneo hilo na Katibu Tawala wa
Wilaya ya Bagamoyo,Erica Yigella ( wa pili kulia) mahali kilipo
Kitongoji cha Uvinje ambapo wakazi wa eneo hilo wamegoma kuhama ndani ya
hifadhi hiyo na wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo
jana. Wa kwanza kulia ni Afisa Wanyamapori, Godfrey Maro na Wa kwanza
kushoto ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Stephano Msumi na pande
wa kulia nyuma ya Katibu Tawala ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa
Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga ( wa pili kulia ) akizungumza na Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa ya Saadani , Stephano Msumi ( katikati) wakati Naibu
Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea
changamoto mbalimbali zinazoikabili . Wa kwanza kulia ni Katibu Tawala
wa Wilaya ya Bagamoyo, Erica Yigella, Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi
wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Vitalis Kuluka, wa tatu kushoto ni Msaidizi
wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga akizungumza jana na Wananchi wa Kitongoji cha
Uvinje ambao wamegoma kuhama ndani ya hifadhi hiyo, wakati Naibu
Waziri huyo alipotembelea kwa ajili ya kuzungumza nao ili kujua ukubwa
tatizo la mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa .
Bango lililopo katika geti la Gama
linalokuelekeza sheria na taratibu ukiwa unaingia katika Hifadhi ya
Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga ( kushoto ) akipatiwa maelezo na Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa ya Saadani , Stephano Msumi ( katikati) wakati Naibu
Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea
changamoto mbalimbali zinazoikabili .Wa kwanza kulia ni Mwakilishi wa
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa, Vitalis Kuluka, nyuma ya Mhifadhi wa Saadani
ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga ( mbele ) akiwa na baadhi ya viongozi wa Hifadhi
za Taifa pamoja kamati ya ulinzi na usalama kutoka Wilayani Bagamoyo
akiongoza kwenda kuangalia sehemu kunakofanyika utalii wa boti katika
Hifadhi ya Taifa ya Saadani wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea
hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali
zinazoikabili .
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kulia) akipatiwa maelezo na Msaidizi
wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu ( wali
kushoto) kuhusiana na sehemu kunakofanyika utalii wa boti katika
Hifadhi ya Taifa ya Saadani . Wengine ni baadhi ya viongozi wa
Hifadhi za Taifa pamoja na kamati ya ulinzi kutoka Wilayani Bagamoyo .
Picha na Lusungu Helela
……………
Wananchi wa Kitongoji cha
Uvinje kilichomo ndani Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani
Bagamoyo Mkoani wa Pwani wamesema hawapo tayari kuhama wala kulipwa
fidia ili kupisha hifadhi hiyo.
Kitongoji hicho, ambacho ni
kati ya vitongoji nane vya Kijiji cha Saadani, kilitakiwa kiondolewe
tangu mwaka 2005 baada ya hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka pori la
akiba na kuwa hifadhi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la
Septemba 16, 2005.
Akizungumza mbele ya kamati ya
Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Bagamoyo, Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga wakati alipofanya ziara jana katika kijiji
hicho aliwambia wananchi hao kuwa lengo la ziara yake ni kutaka
kuwasikiliza juu mgogoro huo na sio kuwahamisha.
‘Mimi ni mgeni kidogo kwenye
Wizara hii, Nimekuja kuangalia sio kuwahamisha kwa kuwa sijui eneo
hili lina ukubwa kiasi na lina kaya ngapi lakini nimekuja kutembelea
hifadhi na maeneo yote yenye changamoto. ‘’ alisema
Alisema amefika kwa ajili ya
kuwasikiliza ili aweze kujua jinsi mgogoro ulivyo kwa sababu hakutaka
kusikia upande mmoja wa TANAPA pekee.
Naye , Kaimu Mwenyekiti wa
Kitongoji hicho, Hassan Akida alisema wakazi wa eneo hilo hawapo
tayari kuhama na wala kulipwa fidia kwa vile ni ardhi yao tokea enzi za
mababu zao.’
‘Tumesema hapa ndo kwetu mnataka kutuhamisha mtupeleke wapi wakati sisi tumezoea maisha yetu hapa’’ alisema Akida.
Aliongeza kuwa kitongoji
hicho kimekuwapo kwa muda mrefu na waliishi bila shida hadi pale pori
hilo lilipobadilishwa na kuwa Hifadhi ya Taifa
“Wakati hili ni pori la akiba
tuliishi vizuri tu na wazazi wetu walikuwa ni wafanyakazi wa pori.
Lakini tangu iwe hifadhi imekuwa taabu. Sasa tunafukuzwa wakati
tumezaliwa hapa na wazazi wetu wamezikwa hapa hapa,” anasema Hassan
Akida.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa
Kijiji cha Saadani, Adam Mwandosi alisema mgogoro huo umedumu kwa
muda mrefu na umekuwa ukileta chuki kati ya Serikali na wananchi.
Amesema wananchi wa eneo hilo
muda mwingine wamekuwa wakimuona hata yeye Mwenyekiti wao kama
anawasaliti kwa vile tokea mgogoro huo ulipoanza viongozi wengi
wamekuwa wakifika hapo lakini wamekuwa hawana majibu ya kumaliza mgogoro
huo.
Mhifadhi Mkuu wa Saadani, Stepahano Msumi amesisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.
Alisisitiza kuwa sheria za hifadhi za Taifa haziruhusu makazi ya watu ndani yake.
“Kwa ufupi tu ukiangalia GN
(Tangazo la Serikali) linaonyesha kuwa eneo lote la kitongoji cha Uvinje
liko ndani ya hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la watu ambao walikuwa
watumishi wa pori la akiba tangu lilipoanzishwa mwaka 1968. Waliombwa
kuondoka lakini waliendelea kuongezeka,” anasema.
Anasema katika makubaliano,
iliamuliwa kuwa walipwe fidia kwa taratibu lakini hata hivyo licha ya
kutekeleza utaratibu wa fidia bado wamegoma kuipokea mbali ya wachache
kujitokeza.
Ikumbukwe kuwa, Saadani ni hifadhi
pekee ya Taifa nchini na Afrika Mashariki yenye fukwe za bahari na
inayotazamana na Bahari ya Hindi na fukwe zake zinakutana na uoto wa
asili wa nchi kavu.
Inapatikana katika mikoa ya Tanga
na Pwani. Uwepo wake ni matokeo ya pori la akiba la Saadani, ranchi ya
Mkwaja na sehemu ya kaskazini, sambamba na akiba ya msitu wa asili wa
Zaraninge.