Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akipata maelezo ya kikundi cha Walemavu kutoka Mwembe Makumbi
kinachojishughulisha na kutengeneza viatu vya ngozi wakati alipotembelea
maonyesho ya walemavu katika uwanja wa Skuli ya Uzini wakati wa
maadhimisho ya siku ya walemavu duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoa
wa Kusini,Unguja.
Sehemu
ya Maandamano ya Walemavu yaliofanyika Uzini, wilaya ya Kati, mkoa wa
Kusini Unguja wakati wa maadhimisho ya siku ya walemavu duniani.
Sehemu
ya Watu wenye ulemavu wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa akihutubia kwenye kilele cha
siku ya kimataifa ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu yaliofanyika
kwenye viwanja vya skuli ya Uzini, wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja,
Zanzibar.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akimkabidhi mafuta maalum ya ngozi Bw. Hussein Ussi Ali wakati wa kilele
cha maadhimisho ya siku ya walemavu duniani katika viwanja vya Skuli ya
Uzini, mkoa wa Kusini Unguja.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akikabidhi kiti maalum cha kutembelea walemavu (Wheel Chair) kwa Bi.
Hidaya Shaib Muombwa ambacho kilipokelewa na ndugu yake kwa niaba wakati
wa kilele cha maadhimisho ya siku ya walemavu duniani katika viwanja
vya Skuli ya Uzini, mkoa wa Kusini Unguja.
Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
……………..
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan ameitaka jamii kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawaachwi
nyuma kwenye nyanja zote za maendeleo.
Makamu
wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watu wenye
ulemavu duniani iliyofanyika mkoa wa Kusini, Unguja, Zanzibar.
Akihutubia
mamia ya watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu kwenye kwenye viwanja
vya Skuli ya Uzini, Makamu wa Rais alisema tumejumuika leo hapa
kuungana na wenzetu duniani kote kuadhimisha kilele cha siku ya
Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani ambayo imebeba kauli mbiu
isemayo “Mabadiliko kuelekea jamii Jumuishi na Maendeleo Endelevu kwa
wote” ujumbe huu unalenga kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu
wanajumuishwa katika mipango yote ya maendeleo ili kuweza kufikia
malengo endelevu ya dunia ifikapo mwaka 2030 pia inakwenda sambamba na
Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020; Ilani ya Chama Tawala na mpango
wa kukuza Uchumi na kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III) ambapo
maswala ya watu wenye ulemavu yamezingatiwa.
Tanzania
iliridhia mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu ambao
umeweka misingi madhubuti wa utekelezaji wa masuala mbali mbali kwa
ajili ya watu wenye ulemavu, ikiwemo; Usawa, Ushirikishwaji kikamilifu
katika mipango ya hifadhi ya jamii na kupunguza umasikini na kuwapatia
huduma pamoja na kufanya kazi na taasisi zinazoshughulikia masuala ya
watu wenye ulemavu, alisema Makamu wa Rais.
Kwa
upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuweka mipango
thabiti na mathubuti yenye kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki
za kisiasa, kiuchumi, kijamii na fursa sawa kama wengine na kuahikisha
watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika ngazi mbali mbaliza
uongozi za kitaifa.
Makamu
wa Rais alitoa rai kwa kusema “kuanzia leo kila mmoja miongoni mwetu
awe askari wa mwenzie katika kuhakikisha kuwa tunalinda haki na usawa wa
watu wenye ulemavu”.
Makamu
wa Rais aliwaasa wanafamilia kutoficha maovu wanayofanyiwa watu wenye
ulemavu, alisema Serikali kwa nguvu zote inakemea vitendo vya ubakaji
na udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu kwani si vitendo vya kiungwana
hata kidogo na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwashughulikia
kikamilifu wahalifu hawa na wakithibitika wafikishwe kwenye vyombo vya
sheria ikiwemo mahakama na kutoa adhabu kali dhidi ya wale
watakaobainika.
Mwisho,
Makamu wa Rais alisema Serikali kwa kushirikiana na Wadau wengine wa
Maendeleo pamoja na wananchi itaendelea kuhakikisha kuwa ‘digital
technology’ inakuwa rafiki kwa walemavu hususan katika kuwawezesha
kupata elimu, vitendea kazi katika maendeo yao pamoja na kuhakikisha
wanafikia kirahisi huduma zote za kijamii.