ALLY AIBUKA MWENYEKITI WA UCHUKUZI SC

December 01, 2017
Bw. Hassan Ahmad (kulia) aliyesimama akiomba kura kwa wapigakura wa klabu ya michezo ya Uchukuzi, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB1).
Katibu aliyemaliza muda wake Bw. Alex Temba akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali mbele ya wapigakura wa klabu ya Uchukuzi kabla ya kufanyika uchaguzi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB1). Aliyeshika chupa ya maji mbele ni Kocha Kenneth Mwaisabula ‘Mzazi’ akimsikiliza kwa makini
Bw. Mbura Tenga (mbele aliyesimama) akimwaga sera zake kwa wapigakura wa klabu ya Uchukuzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).
Wachezaji wa timu ya Uchukuzi wakihesabu kura za Katibu Mkuu mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

      

                       Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI aliyemaliza muda wake wa Klabu ya michezo ya Sekta ya Uchukuzi ,  Mohamed Ally ameshinda kwa kishindo kwa kutetea nafasi yake katika  uchaguzi wa klabu hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Transit wa Jengo la Kwanza la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa (JNIA-TBI) kwa kupata kura 113.
Hatahivyo, Ally pamoja na kupigiwa kura nane (8) za hapana na sita (6) zikiharibika hakuwa na mpinzani baada ya aliyejitokeza awali Bw.Emmanuel  Tumaini kujitoa dakika chache kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa mkutano wa uchaguzi.
Bw. Hassan Ahmad ameshinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura 71 akiwashinda Hamis Mussa (57) na Neema Makassy (8); huku Katibu Mkuu akichaguliwa Mbura Tenga (73) aliyewashinda Katibu aliyemaliza muda wake Alex Temba (46), Ramadhani Kalima (5) na Leonard (2).
Bw. Mrisho Harambe ameweka rekodi kwa kushinda kwa kura 124 katika nafasi ya Katibu Msaidizi ambapo zikiwa ni kura nyingi zaidi walizopata wagombea wengine wa nafasi mbalimbali; na alimshinda Saidi Marusu aliyepata kura nane (8).
Mweka Hazina alichaguliwa Bw. Benjamin Bikulamti (87) aliyemshinda Wilson Magesa (42); huku wajumbe watano waliochaguliwa kutoka katika 14 walioomba kura ni Hilda Mwakatobe (75), Kurwa Sanga (72), Burton Willy (71), Evarist Mmanda (56) na Siraji Silimu (53).

Hatahivyo, Mwenyekiti wa uchaguzi huo Bw. Mputa Maokola amewataka viongozi wapya kudumisha ushirikiano baina yao na wachezaji, na endapo kumetokea matatizo wahakikishe wanasuluhisha ili kuepuka vurugu. Wasimamizi wengine kwenye uchaguzi huo ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Bw. Joseph Matiku kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi) na Mapinduzi Ussi kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).
Akiwashukuru wapigakura kwa niaba ya viongozi wenzake, Makamu Mwenyekiti, Bw.Ahmad amesema wanategemea mchango mkubwa wa mawazo kutoka kwa wanamichezo hao, na kuwataka wawakosoe endapo watakuwa wanakosea.
“Kwa niaba ya wenzangu tutajituma ili kufanikisha lengo letu la ushindi kwenye michezo mbalimbali tutakayoshiriki, lakini mtambue pia tunategemea mchango wenu wa mawazo katika kuendeleza klabu yetu ya Uchukuzi,” alisema Bw. Ahmad.
Hata hivyo, alisema sasa watatengeneza utaratibu wa kufanya wachezaji kukutana mara kwa mara katika michezo ya mabonanza na sio kusubiri michezo ya Mei Mosi na Shimiwi pekee ambayo inafanyika kila mwaka mara moja.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »