Ligi
ya wanawake inatarajia kuanza Jumapili Novemba 26, 2017 kwenye vituo
viwili vya Dar Es Salaam na Arusha ambapo kundi A litakuwa Dar es Salaam
likitumia Uwanja wa Karume wakati kundi B litakuwa Arusha likitumia
Uwanja wa General Tyre.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Dk. Harrison
Mwakyembe kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa uzinduzi
wa Ligi Kuu soka ya Wanawake, imefahamika.
Mbali
ya Dk. Mwakyembe, wageni wengine wanaotarajiwa kuwa katika uzinduzi huo
ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo; Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao
Wilfred pamoja na viongozi wengine wakiwamo Wakuu wa Wilaya mbalimbali
za Arusha na mikoa ya jirani.
Kundi
A lina timu za Mlandizi Queens ya Pwani, JKT Queens ya Dar es Salaam,
Fair Play ya Tanga, Simba Queens ya Dar es Salaam, Ever Green Queens ya
Dar es Salaam na Mburahati Queens ya Dar Es Salaam.
Kundi
B lenyewe linajumuisha timu za Marsh FC ya Mwanza, Kigoma Sisters ya
Kigoma, Panama FC ya Iringa, Baobab Queens ya Dodoma, Alliance Queens ya
Mwanza na Majengo Queens ya Singida.
Ufunguzi
rasmi wa ligi hiyo utafanyika mkoani Arusha Jumapili Novemba 26, 2017
na mchezo wa ufunguzi utakuwa kati ya Panama FC itakayocheza na Alliance
Queens mchezo utakaotanguliwa na hafla ya ufunguzi.
Katika
siku hiyo kituo cha Dar Es Salaam kinachotumia Uwanja wa Karume nako
kutakuwa na mchezo mmoja utakaowakutanisha Mlandizi Queens dhidi ya JKT
Queens.