Wakati Michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam yaani Azam Sports
Federation Cup (ASFC), ikianza kesho Novemba 02, Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), tayari limezilipa timu zote sita zinazoanza
kuchuana hatua ya awali.
Mchezo kati ya Kisarawe United ya Pwani na Silabu ya Mtwara
umeahirishwa hadi hapo baadaye utakapotangazwa tena kwa sababu ya
majeruhi ya wachezaji.
Baadhi ya wachezaji wa Silabu – mabingwa wa Mkoa wa Mtwara wameumia
kutokana na ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Mchinga mkoani Lindi
wakiwa safarini kwenda Pwani.
Mechi zinazotarajiwa kufanyika kesho ni kati ya Buseresere ya Geita
itayocheza na Isako ya Songwe; ilihali Usamala ya Simiyu itacheza na
Sahale All Stars ya Tanga katika mechi hizo za awali kuwania taji la
ASFC.
Baada ya mechi hizo, itakuja Raundi ya Kwanza ya ASFC ambayo
itachezwa kati ya Novemba 7, 8 au 9 ambako TFF imepanga kesho Novemba 2,
mwaka huu kutuma fedha zote za maandalizi ya timu husika ili kusiwe na
kisingizio chochote cha kujiandaa.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred ameagiza Idara ya Fedha na
Utawala ya TFF kulipa fedha hizo haraka, lakini kwa masharti ya taratibu
za malipo kwamba lazima yapitie benki, badala ya akaunti ya mwakilishi
ye yote au kiongozi.
Kidao ameagiza kwamba kwa timu ambayo haijafungua akaunti watakuta
fedha hizo kwenye Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa (FA), lakini TFF
ingependa kusisitiza kwa wadau hao kufufua akaunti au kufungua akaunti
haraka.
Katika raundi hiyo ya kwanza Mashujaa ya Kigoma itacheza na Mshindi
kati ya Buseresere ya Geita na Isako ya Songwe; wakati mechi nyingine
zitakuwa Msange ya Tabora itacheza na Milambo pia ya Tabora ilihali
Bulyanhulu ya Shinyanga itacheza na Area C ya Dodoma.
Kwa mujibu wa droo, Mji Mkuu FC ya Dodoma imeangukia kwa Nyundo ya
Kigoma wakati Baruti FC ya Mara itacheza na Ambassodor ya Kahama,
Shinyanga huku Eleven Stars ya Kagera ikipangwa kucheza na Ndovu ya
Mwanza.
Changanyikeni ya Dar es Salaam itacheza na Reha FC pia ya Dar es
Salaam wakati Mshindi kati ya Kisarawe United na Silabu ya Mtwara
atacheza na Kariakoo ya Lindi huku Cosmopolitan ikicheza na Ajabalo
wakati Makumba FC itapambana na Green Warriors ya Kinondoni wakati
Namungo FC ya Lindi itachuana na Villa Squad ya Dar es Salaam huku Dar
City ikicheza na Majimaji Rangers ua Nachingwea.
Michezo mingine ya hatua ya kwanza itakutanisha timu za Shupavu FC ya
Morogoro na Sabasaba pia ya mjini humo wakati Motochini FC ya Katavi
dhidi ya Ihefu FC ya Mbeya wakati The Mighty Elephant ya itacheza na
Makanyagio ya Rukwa.
Timu ya Burkina FC ya Morogoro itacheza na Mbinga United ya Ruvuma
wakati Makambako Heroes ya Njombe itacheza na Mkamba Rangers ya
Morogoro wakati Real Moja Moja itapambana na African Wonderers – zote za
Iringa. Boma FC ya Mbeya itacheza na African Sports ya Tanga.
Mechi nyingine za hatua hiyo itakuwa ni kati ya Pepsi ya Arusha
ambayo itacheza na Kilimanjaro Heroes ya Kilimanjaro; huku Stand Misuna
ya Singida itacheza na Madini FC ya Arusha ilihali AFC ya Arusha
itacheza na Nyanza ya Manyara wakati New Generation itacheza na Mshindi
kati ya Usamala FC na Sahale ya Tanga. Bodaboda FC itacheza na Kitayose
ya Kilimanjaro.
Michuano hiyo ambayo Bingwa Mtetezi ni Simba SC ya Dar es Salaam,
inashirikisha timu 91 msimu huu kwa mchanganuo wa timu 16 za Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL); 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL); 24 za
Ligi Daraja la Pili (SDL) na 27 za Ligi ya Mabingwa wa Mkoa (RCL).
EmoticonEmoticon