Taasisi
ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) imewezesha warsha ya siku 3
kuwajengea uwezo watafiti wa ndani waweze kuandika andiko bora la
kuombea fedha kwa ajili ya tafiti.
Warsha
hiyo iliyofadhiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Maendeleo
(International Development Research Centre-IDRC) kupitia Jukwaa la
Wanazuoni Wabobezi (Think Tank Initiatives), ilifanyika makao makuu ya
ESRF, Dar es salaam.
Akizungumza
Jijini hapa, Mtalaamu Mwandamizi wa Programu ya Think Tank Initiatives
anayeshughulikia Sera za Uchumi, Dkt. John Okidi kutoka (IDRC), amesema
kwamba watafiti kutoka nchini za Senegali, Tanzania, Uganda, Ghana na
Kenya walikutana kwa siku tatu kujadili na kubadilishana mawazo namna ya
kujenga uwezo katika kuandika maandiko thabiti ya kuomba fedha kutoka
mashirika mbalimbali ya kimataifa.
- Mkuu wa kitengo cha Uwezeshaji na Utawala Bora wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Danford Sango akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki wa warsha ya siku tatu ya uwezeshaji wa maandiko bora ya utoaji ruzuku iliyoandaliwa na ESRF kwa ufadhili wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Maendeleo (IDRC) kupitia Taasisi ya Kimataifa ya Wanazuoni (Think Tank Initiatives-TTI) na kumalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Alisema
kuna umuhimu wa kufanya andiko linaloeleweka ili kuweza kushawishi
watoa ruzuku kutoa fedha za utafiti ili kuharakisha mapinduzi ya viwanda
nchini.
“Watafiti
lazima wawe mstari wa mbele katika kushawishi wanasiasa na viongozi
kutegemea zaidi tafiti katika kuleta matokeo chanya kwa wananchi na
kusukuma umuhimu wa kutumia tafiti katika kufanya maamuzi kwenye ngazi
zote za maamuzi,” aliongeza Dkt. Okidi
Alisisitiza
umuhimu wa utafiti katika utungwaji wa sera za maendeleo ya kiuchumi
hususani katika kipindi hiki ambacho Tanzania inafanya mageuzi makubwa
ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda.
Aliongeza
kwamba Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Maendeleo-IDCR ina programu
ya miaka kumi ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2019.
Alisisitiza
kwamba bila tafiti bora na makini ni vigumu kuwa na sera bora zaidi
katika utatuzi wa changamoto za binadamu katika maeneo mbalimbali hasa
maeneo ya vijijini.
Dkt.
Okidi amesema kwamba watafiti wana umuhimu mkubwa sana katika kushiriki
kwenye ukuaji wa sekta nyingi kama vile gesi, mafuta, biashara na
maeneo mengine ya uwekezaji katika kuongeza tija na mafanikio ya uhakika
baada ya matokeo ya utafiti.
- Picha juu na chini ni Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Uwezeshaji Maendeleo Afrika, Prof. Olu Ajakaiye akielezea namna bora ya utengenezaji wa maandiko kwa ufupi na kwa usahihi wakati wa warsha ya siku tatu ya uwezeshaji wa maandiko ya utoaji ruzuku kwa washiriki kutoka shirika la IPAR- Senegal, Taasisi ya Takwimu, Jamii na Utafiti wa Uchumi (ISSER), REPOA, ESRF, STIPRO na Chuo cha Jamii kutoka Ghana iliyomalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa ESRF.
Mtalaamu
Mwandamizi wa Uwezeshaji Maendeleo na Mafunzo wa Taasisi ya Kimataifa
ya Utafiti wa Maendeleo (IDRC) kupitia program ya TTI , Julie LaFrance,
amesema kwamba ni muhimu kwa watafiti kuendelea na utafiti endelevu na
wa kina ili kuweza kuleta matokeo chanya kwa jamii ya watu baada ya
kupata matokeo baada ya utafiti.
Aliongeza
kwamba baada ya semina hiyo watafiti wa ndani watakuwa wamepata uelewa
mkubwa wa kuandika mapendeko thabiti na bora zaidi yenye kuvutia wadau
wa maendeleo na mashirika ya kimataifa kuanza kuwapa fedha kwa ajili ya
tafiti zenye tija nchini.
Warsha hiyo pia iliwakutanisha watafiti kutoka Taasisi ya IPAR- Senegal, Taasisi ya Takwimu, Jamii na Utafiti wa uchumi (ISSER), REPOA, ESRF, STIPRO na chuo cha Jamii kutoka Ghana.
- Mkuu wa Idara ya Utafiti na Machapisho wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene (kulia) akibadilishana mawazo na Mtalaamu Mwandamizi wa Uwezeshaji Maendeleo na Mafunzo wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Maendeleo (IDRC), Julie LaFrance wakati warsha ya siku tatu ya uwezeshaji wa maandiko ya utoaji ruzuku iliyoandaliwa na ESRF kwa ufadhili wa IDCR kupitia Think Tank Initiatives-TTI.
EmoticonEmoticon