Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akisalimiana na badhi ya
watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera alipowasili
katika Ofisi hiyo ili kuzungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na watumishi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera kuhusu masuala ya
kiutendaji alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo
Mkoani humo.
Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
(TRA) Mkoani Kagera, Bw. Adam Ntoga, akiwasilisha taarifa ya utendaji ya
Mamlaka hiyo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb) alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo
Mkoani Kagera.
Baadhi ya Maafisa wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera wakimsikiliza kwa makini Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo
pichani) alipokuwa akizungumzia kuhusu uadilifu katika kazi na utoaji wa
elimu kwa mlipakodi baada ya Naibu Waziri huyo kufanya ziara ya kikazi
katika Ofisi hiyo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati) akizungumza na viongozi pamoja
na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera,
alipofanya ziara ya kikazi katika Mkoa huo ambapo amewaasa kuwa
waadilifu katika kazi zao.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati -walioketi) akiwa katika picha ya
pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera
na baadhi ya Maafisa Waandamizi katika Mkoa huo.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa
wa Kagera Bw. Seif Mkude (kulia) akielezea kuhusu utayari wa
wafanyabiashara wa Mkoa huo kulipa kodi wakati wa Mkutano kati ya
wafanyabiashara wa Mkoa huo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati).
Mfanyabiashara wa Mkoa wa Kagera
Bw. Taimur Manyilizo, akieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo
wafanyabiashara Mkoani humo ikiwemo kile alichoeleza uwepo wa taasisi
nyingi zinazodai kodi nyingi ikiwemo OSHA, TFDA, Zimamoto ambapo
aliiomba Serikali iziangalie na kuzifanyia kazi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akizungumza kuhusu ushirikiano
kati ya Serikali na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera katika kukuza
Uchumi wa nchi baada ya Naibu Waziri huyo kufanyaziara ya kikazi Mkoani
humo.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – WFM
………………….
Benny Mwaipaja, KAGERA
Serikali imelipa madeni ya
wazabuni, wakandarasi na malimbikizo ya wafanyakazi yanayofikia kiasi
cha shilingi bilioni 190 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai
hadi Septemba mwaka huu baada ya kufanya uhakiki wa madeni halali
inayodaiwa na wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali.
Hayo yamesemwa Mjini Bukoba mkoani
Kagera na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dokta Ashatu Kijaji
(Mb), wakati akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa mkoa huo akiwa
katika ziara ya kikazi kukagua utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).
Dokta Kijaji alisema kuwa wazabuni
wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 67.2, wakandarasi wamelipwa
shilingi bililioni 24.2, watoa huduma mbalimbali wamelipwa Shilingi
bilioni 38, watumishi wa umma wamelipwa Shilingi bilioni 37, huku wadai
wengine wakilipwa shilingi bilioni 24.
Alisema kuwa katika bajeti ya
mwaka 2016/2017, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi trilioni 1 kwa
ajili ya kulipa madeni mbalimbali na kwamba itaendelea kulipa madeni
yote yaliyohakikiwa.
Dkt. Kijaji aliiambia Jumuiya ya
Wafanyabiashara mkoani Kagera kwamba Serikali inatambua mchango wao
mkubwa katika maendeleo ya Taifa kutokana na kulipa kodi zinazochangia
kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za jamii.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara
kutumia mashine za kielektroniki katika biashara zao, kutoa stakabadhi
wanapouza bidhaa na huduma huku wananchi wakiaswa kudai stakabadhi
wanapofanya manunuzi ya aina yoyote na kuhakikisha kuwa stakabadhi hizo
zinaonesha kiasi halisi walicholipia huduma na bidhaa walizonunua.
Akizungumza kwaniaba ya Jumuiya ya
Wafanyabiashara mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bw. Seif
Mkude, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna
inavyohamasisha na kushikia bango masuala ya kodi kwa manufaa ya Taifa.
Alisema kuwa wafanyabiashara
wameridhika na namna kodi wanazolipa zinavyosimamiwa kikamilifu na
kutekeleza miradi dhahiri ya maendeleo na kuahidi kuwa wataendelea
kulipa kodi hizo ili kujenga uchumi wa nchi.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara
wenzake kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuunga mkono juhudi za Mhe.
Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli huku akiishauri Serikali kuondoa
kero ndogondogo zilizotolewa na wafanyabiashara wakati wa mkutano huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa
mkoa wa Kagera, Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus Kinawiro,
aliwashauri wafanyabiashara hao kupanua wigo wa biashara zao ili waweze
kunufaika na uwepo wa soko huru katika nchi zaidi ya nne zinazopakana na
mkoa huo ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, DRC Kongo, Kenya na nchi
nyingine.
EmoticonEmoticon