RC SHIGELLA :SERIKALI ITAENDELEA KUNYAG'ANYA MASHAMBA NA VIWANDA AMBAVYO VIMESHINDWA KUENDELEZWA

October 31, 2017
 MKUU wa Mkoa wa Tanga,Martini Shigella akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara kwenye shamba la mkonge la Mkumbara kulia ni Mmiliki wa Shamba hilo,Damian Ruhinda na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo D.D Ruhinda Deogratius Ruhinda

 MKUU wa Mkoa wa Tanga,Martini Shigella wa pili kutoka kushoto akiangalia maeneo mbalimbali kwenye shamba hilo
 MKUU wa Mkoa wa Tanga,Martini Shigella wa pili kutoka kulia akiangalia bidhaa zinazozalishwa na shamba hilo kushoto ni
Mmiliki wa Shamba hilo,Damian Ruhinda
 MKUU wa Mkoa wa Tanga,Martini Shigella katikati akiangalia namna mkonge unavyozalishwa kulia ni Mmiliki wa Shamba hilo,Damian Ruhinda kushoto ni  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo D.D Ruhinda Deogratius Ruhinda
MKUU wa Mkoa wa Tanga,Martini Shigella kushoto aliyeshika zao la mkonge akimsikiliza kwa umakini Mmiliki wa Shamba la Mkonge la Mkumbara wilayani Korogwe Mkoani Tanga Damian Ruhindawakati alipofanya ziara ya kulitembelea

                               Yusuph Mussa,Korogwe.
 
MKUU wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela amesema Serikali itaendelea kunyang'anya  mashamba na viwanda ambavyo vimeshindwa kuendelezwa na kupewa wawekezaji wengine kama walivyofanya kwa baadhi ya mashamba ya wilaya ya Muheza na sasa wamechukua Shamba la Mkonge Mnazi wilayani Lushoto.

Nia ya Serikali ni kuona wawekezaji wazawa na wageni wanawekeza kwa tija kwenye viwanda, makampuni na mashamba makubwa ili wao wanufaike kwa wananchi kupate ajira na serikali ipate kodi.

Aliyasema hayo  alipofanya ziara kwenye Kiwanda cha Mkonge Mkumbara kilichopo Kata ya Mkumbara, Tarafa ya Mombo wilayani Korogwe chini ya Kampuni ya D.D. Ruhinda inayomilikiwa na Damian Ruhinda.

Shigela alisema uwekezaji aliouona kwenye kiwanda hicho ambacho kina shamba lenye ukubwa wa eneo la mraba la hekta 1,700, ni mkubwa na unatakiwa kuwa mfano kwa wawekezaji wengine hasa wazawa, ambapo kwa kiwanda hicho cha mkonge kuzalisha kwa tija, wananchi na Serikali wanapata.

"Uwejezaji unaofanywa na Ruhinda ndiyo unaotakiwa kuoneshwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Kwani tunachokitaka Serikali ni kuona wananchi wanaofanya kazi kwa mwekezaji huyo wanapata neema na sisi Serikali tunachukua kodi, na hilo ndilo linafanyika hapa, ambapo zaidi ya wafanyakazi 300 wameajiriwa.

"Tunapenda kutoa tahadhari kwa wawekezaji kuwa Serikali msimamo wake upo pale pale, kiwanda, kampuni au shamba lisiloendelezwa tunalichukua na kumpa mtu mwingine, kama tulivyofanya kwa Shamba la Mkonge Mnazi (lipo Wilaya ya Lushoto), ambapo baada ya mwekezaji kushindwa kuliendesha Serikali tumelichukua" alisema Shigela.

Shigela alisema shamba hilo lenye hekta 5,000, hawawezi kulibadilishia matumizi, bali litaendelea kuzalisha mkonge, kwani malighafi ya mkonge na mitambo yake vyote vipo, na amempa ofa Ruhinda aweze kwenda kununua shamba hilo na kuweza kuendeleza zao la mkonge.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayomiliki kiwanda na Shamba la Mkonge Mkumbara Deogratius Ruhinda alisema moja ya changamoto kwao ni mlolongo wa kodi ambazo zinashikwa na watu tofauti ikiwemo Taasisi ya Osha, ambayo ipo kwa ajili ya kuangalia usalama wa wafanyakazi kazini.

"Kodi nyingine inachukuliwa na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na halmashauri. Kama tungepewa nafasi ya kutoa maoni yetu, ningeshauri kodi ikusanywe na mtu mmoja ambaye ni TRA. Hiyo ingetusaidia kupata unafuu mkubwa, na kuweza kupata faida kile tunachozalisha. Lakini pia tuwalipe vizuri wafanyakazi wetu na tuweze kulipa kodi serikalini" alisema Ruhinda.

Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni  ya D.D. Ruhinda, Damian Ruhinda, alimuomba Mkuu wa Mkoa amueleze Rais Dkt. John Magufuli aweze kufanya ziara ya kutembelea wadau wa mkonge mkoa wa Tanga, kwani kwa sasa wamebaki wawekezaji wazalendo tofauti na wale wa zamani maarufu kama mabepari.

"Pamoja na mafanikio yetu tangu tuliponunua haya mashamba ya mkonge kutoka serikalini, bado tuna changamoto nyingi, hivyo Mkuu wa Mkoa tunakuomba mueleze Rais aweze kutembelea mashamba na viwanda vyetu... sisi tunamuunga mkono kwa asilimia 100 nchi hii kuwa ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025" alisema Ruhinda.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »