Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said
amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda,
uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi
na mafuta na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza
uchumi kwa kasi zaidi.
Ujumbe huu wa Mfalme wa Oman umewasilishwa kwa Mhe. Rais Magufuli
na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al
Rumhy aliyeongozana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben
Nasser Al Ismaily na Naibu Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid, Ikulu
Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Rumhy ambaye ameongoza watu zaidi 300 waliokuja nchini kwa meli
ya Mfalme wa Oman amesema ziara hii imelenga kuimarisha uhusiano kati
ya Tanzania na Oman hususani katika masuala ya uchumi, ambapo Oman
inabadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi,
itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji
wa Bagamoyo, itajenga viwanda vya mazao na kununua mazao ya wakulima
na itawekeza katika uchakataji wa madini ili kuongeza thamani.
“Mhe. Rais tunataka kushirikiana nanyi kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa
Bagamoyo, tunataka Bagamoyo isiwe eneo la bandari tu, bali pia liwe ni eneo
ambalo tutajenga viwanda mbalimbali, tuzalishe mbolea na tununue mazao ya
wakulima na kuyasafirisha, sisi tupo tayari na kesho tunakwenda kuangalia eneo
hilo ili kazi zianze mara moja” amesema Dkt. Rumhy.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Oman
Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said kwa kutuma ujumbe huo na
amemhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi
uhusiano wake na Oman.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Rumhy kufikisha ujumbe wake kwa
Mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo
unaanza mara moja na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote
utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Mhe. Dkt. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa
ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania, nimefurahi kuona mpo tayari
kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa
uwekezaji wa Bagamoyo, sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane kwa sababu
nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote” amesema Mhe.
Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na
Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika
usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana
wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili
na Kiarabu.
Amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada kujenga visima vya maji 100
hapa nchini na amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya
kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya
ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt.
Medard Matogoro Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Alphonce Kolimba.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Oktoba, 2017
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al
Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam
leo Oktoba 18, 2017.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben Nasser Al
Ismaily aliyeongozana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed
Hamad Al Rumhy alipokutana na kufanya nao mazungumzo Ikulu jijini Dar
es salaam leo Oktoba 18, 2017.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Naibu Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid
aliefuatana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al
Rumhy walipokutana na kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo
Oktoba 18, 2017.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Balozi wa Oman nchini Mhe.Ali A. Al Mahruqi
aliyefuatana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al
Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam
leo Oktoba 18, 2017.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
katika mazungumzo na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad
Al Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es
salaam leo Oktoba 18, 2017.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika
picha ya kumbukumbu na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed
Hamad Al Rumhy na ujumbe wake baada ya kukutana na kufanya naye
mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsiliza
Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy akiongea na
wanahabari baada ya kukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini
Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017.
EmoticonEmoticon