Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na wananchi waliokuwa wamepanga foleni
kulipa ushuru katika mnada wa Malendi Wilayani Iramba.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akikagua mnada wa Malendi Wilayani Iramba ambapo
amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha anajenga vyoo na
kufikisha huduma za maji ndani ya mwezi mmoja.
Baadhi ya wananchi wa
Kijiji cha Malendi na maeneo ya jirani waliokuwa katika mnada huo wakinyoosha
mikono kumsalimia Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi alipowatembelea
mnadani hapo.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi amempa mwezi mmoja Mkurugenzi wa halmashauri ya
Wilaya ya Iramba, kujenga vyoo bora katika Mnada uliopo Kijiji cha Malendi,
kata ya Mgongo Wilayani humo.
Dkt Nchimbi ametoa
agizo hilo mara baada ya kutembelea mnada huo ambapo wananchi wamelalamika
kukosa huduma za vyoo na maji kwa kipindi kirefu huku halmashauri ikikusanya
ushuru bila kuwaboreshea miundombinu ya mnada huo.
“Mkurugenzi nakupa
mwezi mmoja hapa kuwe na vyoo bora vikiwa na matundu sita kwa ajili ya wananchi
hawa pamoja na huduma za maji, kipindi cha mvua kinaanza, lazma muwajali
wananchi hawa kwakuwa kipindupindu kinaweza kulipuka hapa”, ameeleza Dkt
Nchimbi.
Ameongeza kuwa kwakuwa
hakuna vyoo wananchi watajisaidia maeneo ya jirani na mnada na mvua zikianza
zitatiririsha uchafu huo katika eneo la mnada na makazi ya wanakijiji cha
Malendi na hivyo kusababisha mlipuko wamagonjwa hasa Kipindupindu.
Dkt Nchimbi amesema
Mkurugenzi huyo ajenge vyoo vyenye matundu sita pamoja na kuvuta huduma za maji
kwakuwa maji husaidia usafi wa eneo hilo na kupunguza uwezekano wa magonjwa
hayo.
“Halmashauri mna
jukumu la kuhakikisha mnada huu una miundombinu yote hasa ya maji na vyoo
kwakuwa mnakusanya ushuru pia kumbukeni kuhakikisha huduma zinapatikana vizuri
mnadani hapa”, ameelekeza Dkt Nchimbi.
Aidha amewataka
Wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na idara za
usafi wa mazingira na Wakala wa barabara vijijini (TARURA) wanahakiki njia na
mitaro ya kupitisha maji ili mvua zisilete maafa pamoja na kuhakiki mabwawa ili
baada ya mvua kuisha waweze kuvuna maji ya kutosha.
Dkt Nchimbi ameeleza
kuwa mvua za msimu uliopita zilileta maafa ya kipindupindu hivyo hatarajii kwa
mvua za msimu huu kuleta tena magonjwa kwakuwa wakurugenzi wametahadharishwa
mapema uwepo wa mvua za wastani na juu ya wastani.
Ameongeza kwa
kuwashauri wananchi kuimarisha makazi yao ili yaweze kuhimili mvua hizo pamoja
na kujenga vyoo bora ili wasipate magonjwa hasa kipindupindu.
Naye Kaimu Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Iramba Marietha Kasongo amesema amelipokea agizo hilo na
kuongeza kuwa mwezi mmoja unatosha kujenga vyoo hivyo na kufikisha huduma za
maji mnadani hapo.
Amesema halmashauri
ilikuwa na mpango wa kujenga vyoo na kuvuta maji mnadani hapo hivyo agizo la
Mkuu wa Mkoa limewaamsha ili waweze kutekeleza mipango yao kwa haraka zaidi.
Awali Mamlaka ya Hali
ya Hewa nchini imetangaza kuwa Mkoa wa Singida unatarajiwa kupata mvua za
wastani na juu ya wastani, aidha wastani wa mvua kwa Mkoa wa Singida ulikuwa ni
Milimita 500 mpaka 850.
EmoticonEmoticon