Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akimpa maelekezo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya United Builders Ltd, Harshad Patel (kushoto) ambayo inajenga mradi wa bweni na ukumbi wa mihadhara katika Chuo cha Misitu Olmotonyi alipotembelea chuo hicho jana mkoani Arusha. Aliitaka kampuni hiyo iharakishe kumaliza ujenzi wa mradi huo.
Na Hamza Temba - WMU
.................................................................
Chuo cha Misitu Olmotonyi kilichopo mkoani Arusha kimetakiwa kuboresha taaluma na mitaala ya kufundishia iweze kukidhi mahitaji ya jamii ya sasa na ijayo ikiwemo kujibu kero na changamoto zinazoikabili jamii hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alipotembelea chuo hicho jana kwa ajili kukagua maendeleo yake na kuzungumza na waalimu pamoja na wafanyakazi ambapo pia alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayojengwa chuoni hapo ikiwemo ya bweni na ukumbi wa mihadhara.
Alisema Tanzania ya leo inahitaji wataalamu watakaojibu kero na kutatua changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya uhifadhi nchini ikiwemo ya uharibifu wa misitu kwa njia ya uchomaji wa mkaa, uvunaji haramu wa magogo na vitendo vya uingizaji wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini.
"Ni lazima muwafundishe wanafunzi wenu uaminifu na uzalendo wa kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu, muwafundishe uhifadhi zaidi na sio uvunaji pamoja kutumia sheria ipasavyo katika kulinda na kusimamia rasilimali hizi huku wakitambua kuwa rasilimali hizo zikitoweka hakuna maisha kutokana na umuhimu wake katika maisha ya binadamu" alisema Prof. Maghembe.
Pamoja na hayo, alikitaka chuo hicho kujiimarisha zaidi katika mafunzo kwa vitendo kufikia viwango bora vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kuendeleza waalimu kitaaluma kwa kutumia fursa mbalimbali ikiwemo za mafunzo ya nje ya nchi kwa mfumo wa "Scholarships".
Aidha, alikitaka pia chuo hicho kujikita zaidi katika utoaji wa huduma kwa jamii katika sekta ya misitu pamoja na kuanzisha na kuimarisha programu mbalimbali za utafiti ambazo pamoja na faida nyingine pia zitakitangaza chuo hicho ndani na nje ya nchi.
Katika
hatua nyingine, Prof. Maghembe amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya United
Builders Ltd, Harshad Patel kukamilisha haraka ujenzi unaoendelea wa jengo la
bweni na ukumbi wa mihadhara chuoni hapo. Ujenzi huo upo chini ya mradi wa
ECOPRC na jengo la bweni litakua na uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 na ukumbi
wa mihadhara wanafunzi 200.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Christognus Haule alisema, chuo hicho kinatoa mafunzo ya misitu na hifadhi ya mazingira kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada pamoja na mafunzo ya muda mfupi. Pia kinatoa huduma za ushauri na utafiti wa misitu na hifadhi ya mazingira.
Akizungumzia udahili wa wanafunzi chuoni hapo alisema umekua ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2015/2016 idadi hiyo imeongezeka kutoka 499 na kufikia 595 mwaka 2016/2017. Alisema kwa mwaka ujao 2017/2018 wanategemea kupata wanafunzi wengi zaidi kufikia 650.
Chuo cha Misitu Olmotonyi ni chuo cha Serikali ambacho kilianzishwa mwaka 1937 na kinasimamiwa na Wizara ya Maliasili kwa ajili ya kutoa mafunzo ya misitu na hifadhi ya mazingira. Chuo hicho kwa sasa kina waalimu 21 wa ngazi tofauti.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya United Builders Ltd, Harshad Patel ambayo inajenga jengo la bweni na ukumbi wa mihadhara katika Chuo cha Misitu Olmotonyi kuhusu maendeleo ya mradi huo alipotembelea chuo hicho jana mkoani Arusha. Aliitaka kampuni hiyo iharakishe kumaliza ujenzi wa mradi huo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Chuo cha Misitu Olmotonyi Mkoani Arusha jana ambapo alitoa maelekezo mbalimbali na ushauri wa kuboresha chuo hicho. Kulia ni Mkuu wa Chuo hicho, Christognus Haule.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe (kushoto) akizungumza na wafanyakazi wa Chuo cha Misitu Olmotonyi Mkoani
Arusha alipofanya ziara ya kikazi chuoni hapo jana ambapo alitoa maelekezo na
ushauri wa namna ya kuboresha chuo hicho.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza na waalimu na wafanyakazi wa Chuo cha Misitu Olmotonyi mkoani Arusha jana . Kulia kwake ni Mkuu wa Chuo hicho, Christognus Haule.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia waliokaa) na baadhi ya wafanyakazi wa Chuo cha Misitu Olmotonyi.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia waliokaa) na baadhi ya waalimu wa Chuo cha Misitu Olmotonyi.
Ujenzi bweni la wanafunzi chuoni hapo ukiwa unaendelea chini ya mradi wa ECOPRC.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe (wa pili kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya United Builders Ltd, Harshad Patel (kulia) ambayo inajenga jengo la bweni na ukumbi wa mihadhara katika Chuo cha Misitu Olmotonyi kuhusu maendeleo ya mradi huo
alipotembelea chuo hicho jana mkoani Arusha. Aliitaka kampuni hiyo iharakishe
kumaliza ujenzi wa mradi huo.
Jengo la vukumbi wa mihadhara (Lecture Theatre) ambalo linaendelea kujengwa chuoni hapo kupitia mradi mradi wa ECOPRC.
Baadhi ya waalimu na wafanyakazi wa Chuo cha Misitu Olmotonyi wakisikiliza maelekezo mbalimbali kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (hayupo pichani) alipotembelea chuo hicho jana mkoani Arusha.
Baadhi ya waalimu na wafanyakazi wa Chuo cha Misitu Olmotonyi wakisikiliza maelekezo mbalimbali kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (hayupo pichani) alipotembelea chuo hicho jana mkoani Arusha.
EmoticonEmoticon