Rais wa Kwanza wa Bunge la Afrika, Getrude Mongela amesema wakati umefika kwa wanawake kuajiri na kufukuza.
Alitoa
kauli hiyo katika sherehe za Uzinduzi wa Jukwaa la Kuwaendeleza
Wanawake Afrika (WAA) iliyofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini
Dar es Salaam. Jukwaa hilo linasimamiwa na Taasisi ya Graca Machel.
Mama
Mongela alikuwa akijibu maswali ya waandishi kuhusiana na hisia zake
baada ya uzinduzi na majadiliano ya Kitabu “Women Creating Wealth”
ambazo ni simulizi la wanawake wajasiriamali katika bara la Afrika,
waliofanikiwa na safari yao katika ujasiriamali.
Alisema
ingawa wakati wa Mwalimu Nyerere juhudi zilifanyika kuwawezesha
wanawake, kundi hilo lilibaki kufanyakazi za kufungasha au kushona,
lakini kizazi cha sasa kimeendelea kiasi ya kwamba kina uwezo wa kufanya
uwekezaji na kuwa waajiri.
- Rais wa Kwanza wa Bunge la Afrika, Getrude Mongela akifanya mahojiano na mwandishi wa kituo cha Televisheni cha ITV, Henry Mabumo mara baada ya uzinduzi wa kitabu cha Kitabu “Women Creating Wealth” wakati wa sherehe za Uzinduzi wa Jukwaa la Kuwaendeleza Wanawake Afrika (WAA) iliyofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. Jukwaa hilo linasimamiwa na Taasisi ya Graca Machel.(Picha zote na Thebeauty.co.tz)
Alisema
amefurahishwa sana na maelezo ya ndani ya kitabu hasa safari mbalimbali
za wanawake kuanzia vijana na wale wa kati ambao wamethubutu na
kuonesha njia ya ujasiriamali bila kukata tamaa na hivyo kuwa mfano kwa
wengine.
Alisema
katika mahojiano hayo kuwa wanawake kwa sasa wakati umefika wa kuwa na
viwanda vikubwa, kumiliki na kuwezesha mabadiliko ambayo yatachochea
maendeleo binafsi, familia na hata taifa.
Anasema
wanawake waliachwa nyuma kutokana na wanaume kutotambua au kutokubali
uwezo wa mwanamke na sasa vijana wanaonesha kwamba wanawake wanaweza na
wanathubutu.
Pamoja
na kazi hizo amesema wakati umefika wa wanawake kutumia akili ili siku
moja kipuri kitengenezwe na mdada na watu wajisikie fahari kwenda
kukitumia.
Akizungumzia
kitabu hicho Mwasisi wa mtandao wa She Inspires Her, Lisa
O'Donoghue-Lindy amesema kwamba kinatoa maelezo ya safari ya
wajasiriamali wa kike, dhiki zao, changamoto na namna walivyoanzisha
ujasiriamali wakati mwingine wakiwa na fedha kidogo kiasi cha dola 23
katika mifuko yao.
Alisema
kitabu hicho kimeandaliwa kutoka wajasiriamali mbalimbali takribani 60
wa bara la Afrika kwa lengo la kutoa hamasa kwa wajasiriamali wengine
ambao wanachipukia au wale ambao wanataka kuthubutu.
Alisema
kwamba maelezo yaliyomo ndani ya kitabu hicho ni binafsi mno, kwani
walizungumzia ubunifu na safari ya kiuchumi waliyoianzisha wadada hao na
namna waliyvoondoka katika changamoto mbalimbali. Aidha kimelenga
kushawishi watoa maamuzi kutoa nafasi ya wanawake kuendelea na kuona
umuhimu wao katika kuimarisha maendeleo na usawa.
Miongoni
mwa watu waliomo ndani ya kitabu hicho Jacqueline Mengi, Esther Karin
Mngodo, Devotha Minzi na Mtendaji wa kampuni ya uhandisi ya Mount Carmel
Seline Mwenelupembe. Wapo pia wajasiriamali kutoka Kenya, Uganda na
Kongo ya Kinshasa.
Akizungumza
kuhusu kuwamo katika kitabu hicho Jacqueline Mengi alisema anajisikia
furaha kuwa mfano wa kuwafundisha wengine, akisema kwamba anaona fahari
kuwaambia wanawake wenzake kwamba kujiamini ni silaha muhimu na kwamba
ukishinda nafsi ni lazima ufanikiwe.
Aliwataka wanawake kushikamana na kupeana ushirikiano katika safari hiyo.
Naye
Renee Ngamau Mtangazaji wa redio kipindi cha Capital in the Morning
kutoka kampuni ya Capital Group Limited alitoa hongera kwa kukazabuti
kwa washiriki wote waliomo katika kitabu kwamba wamefanyakazi moja
muhimu ya kuonesha wanawake kwamba ujasiri na uthubutu ni kitu cha
muhimu katika kuamua maisha yao binafsi. Alisema wanawake hao wameonesha
kwamba kwa hali yoyote ile mwanamke akifanya maamuzi ya kuendelea mbele
ataweza.
Anasema
wanawake ndio msingi mkubwa wa maendeleo kwa kuwa asilimia 90 ya pato
lao hulirejesha katika familia kwa shughuli mbalimbali za kijamii.
Akielezea
siri ya mafanikio yake Devotha Minzi ambaye kwa sasa ana kampuni ya
ushauri kuhusu namna ya kuingia katika ujasiriamali, alisema kwamba
mambo ambayo yamekuwa yakimfikirisha sana ni kuhusu namna ya wahitaji
wanavyoweza kupata fedha benki na wala si benki kutoa fedha.
Minzi
ambaye aliwahi kuajiriwa Benki Kuu aliacha kazi yake hiyo na kuingia
katika kuwekeza katika taasisi ya fedha kabla ya kuachana nayo na
kuanzisha kampuni ya ushauri.
Akizungumza
katika mkutano huo alisema kwamba wakati anaingia katika ujasiriamali
alitambua kwamba kuna shida ya kujiweka sawa kuchukua fedha za Benki na
hivyo kuona haja ya kuwapa elimu wanawake kuhusu Benki kuwapa fedha na
si kunung’unika kwamba hawapewi fedha.
Alisema
ni vyema wanawake kufanyakazi zao kwa akili zaidi na kuhakikisha kwamba
wamejiandaa vyema katika kuhakikisha kwamba mahitaji yao yanatekelezeka
kwa kutambua mambo ambayo ni muhimu katika uwekezaji na kuwa na nguvu.
Anasema
mpaka alipofika yeye amekumbana ana changamoto nyingi lakini la maana
ni kuwa ana ratibu na anaangalia zaidi mahitaji na taratibu zake
akiongeza kwamba kwa sasa amejikita kutoa ushauri wa kuwawezesha
wanawake wenzake kukopesheka.
Alisema ni vyema watu wakabadilika kifikra na kutengeneza utaratibu ambao utawafanya benki wawape hela bila hata kuombwa.
Katika
jukwaa hilo wanawake walipata nafasi pia ya kuhutubiwa na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye
aliwataka wanawake kusaidia serikali katika kuhakikisha uchumi unakua.
- Rais wa Kwanza wa Bunge la Afrika, Getrude Mongela (aliyeipa mgongo kamera) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Amorette Ltd, Jacqueline Mengi (wa tatu kushoto) Mkurugenzi wa Shule Direct, Faraja Nyarandu (wa pili kushoto), Mmiliki wa duka la ENJIPAI, Nasreen Kareem (kushoto) wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu cha “Women Creating Wealth” uliofanyika jijini Dar es Salaam.
EmoticonEmoticon