Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) na Taasisi ya kupigania uhai wa maisha ya wanyama wa
mbugani ya Wildaid Alhamisi Mei 4, mwaka huu kwa pamoja wamesaini
makubaliano ya vita dhidi ya ujangili.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwakilishi wa taasisi hiyo, Lily Massa.
Akizungumza kabla ya kusaini
makubaliano hayo, Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema kwamba, “Hii ni
sehemu nyingine ya TFF kujihusisha na shughuli za kijamii licha ya kuwa
na majukumu ya kusimamia maendeleo ya mpira wa miguu katika kukuza na
kuendesha mashindano.”
Malinzi amesema TFF
inaendeleza utamaduni wa shughuli mbalimbali za jamii kwani hata kwa
Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Tenga enzi za utawala wake akiwa
kiongozi mkuu wa mpira wa miguu, alifanya hivyo katika kampeni za
kupinga maambukizi mapya ya UKIMWI.
“Wengi mtakumbuka kuwa
kulikuwa pia na vita vya kupigania afya za watoto na kupigania uhai wao
pia kampeni za amani ambazo mpira wa miguu umetumika kuelimisha,”
amesema.
Kwa hatua hii ya sasa, Rais
Malinzi amesema kwamba TFF, inaingia makubaliano hayo na kuiteua timu ya
taifa ya vijana Tanzania maarufu kama Serengeti Boys kusimama kidete
kupinga uwindaji haramu wa wanyama mbugani kwa kuwa ni hazina kubwa kwa
vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wa Mwakilishi wa
WildAid, Lily Massa, alishukuru kuingia kwa makubalino hayo akisema
kwamba ndoto zao za kupiga vita uwindaji haramu na ujangili,
itafanikiwa.
“Tunashukuru kuingia programu
hii na ninaamini Mungu atatusaidia,” amesema Massa ambaye taasisi yake
iko karibu kila nchi yenye wanyama wa mbugani.
Katika hatua nyingine, Rais
Malinzi aliitakia kila la kheri Serengeti Boys ambayo kwa sasa
inajiandaa kuingia Gabon kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Mei 14, mwaka huu ambako
Serengeti Boys ambayo iko Kundi B itakuwa Libreville – Mji Mkuu wa
Gabon. Timu nyingine za Kundi B ni Mali, Niger na Angola