Naibu
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB)
(mwenye tai) akikaribishwa katika Banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo
ya Tanzania (TADB) mara baada ya kufungua Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki
ya Maziwa inayofanyika Kitaifa mjini Bukoba, mkoani Kagera kuanzia
tarehe 28 Mei had Juni 01.
Wito
umetolewa kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) kuwafikia
wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo nchi nzima ili kuweza kuwakwamua
katika changamoto zinazorudisha nyuma juhudi zao za kujiongezea kipato
kwa kukosa mitaji ya uhakika katika kuongeza tija ya kilimo nchini.
Wito
huo umetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa
William Tate Ole Nasha (MB) wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya
Kampeni ya Wiki ya Maziwa inayofanyika Kitaifa mjini Bukoba, mkoani
Kagera.
Mhe.
Ole Nasha amesema kuwa dhima ya kuanzishwa kwa TADB ni kutoa suluhisho
la ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha na mikopo kwa wakulima wadogo
nchini ili kuchagiza maendeleo ya kilimo nchini hivyo Benki ina wajibu
wa kuwafikia wakulima wote wadogo wenye uhitaji wa mikopo.
“Nawaomba
mujielekeze kutoka mikopo yenu ya gharama nafuu kwa wakulima wadogo
ambao hawawezi kupata mikopo kwenye benki za biashara ili kutekeleza
lengo la Serikali la kuwainua wakulima kutoka kilimo cha kujikimu kwenda
cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza
umaskini nchini,” Mhe. Ole Nasha alisema.
Aliongeza
kuwa anafahamu kuwa Serikali ikishirikiana na TADB ilifanya mazungumzo
na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kupelekea Bodi ya Benki ya
Maendeleo Afrika kutoa kibali cha kuipatia TADB fedha za kukopesha
kwenye sekta ya kilimo, na kuitaka Benki hiyo kutumia fedha hizo kwa
kuwapatia wakulima wadogo ambao ni wahitaji zaidi wa miko hiyo.
“Naomba muwakopeshe wakulima hizo fedha ya zaidi Bilioni 200 ili kuwaongezea tija katika shughuli zao,” aliongeza.
Kwa
mujibu wa mpango kazi wa TADB hadi kufikia miaka mitano ijayo itakuwa
imefungua ofisi sita za kikanda zenye lengo la kuwahudumia wakulima wote
nchini. Ambapo katika hatua za awali Benki hiyo inaendelea kuwajengea
uwezo wakulima wa nchi nzima ili kuwaandaa kupata mikopo kutoka Benki
hiyo.
Mpango
kazi huo unaweka bayana malengo mengine yanayojumuisha utafutaji wa
fedha toka vyanzo mbalimbali zenye gharama nafuu kwa minajili ya
kuwakopesha Wakulima katika hatua zote za mnyororo wa ongezeko la
thamani kwenye mazao ya Kilimo na kupanua wigo wa utaoji mikopo toka
Minyororo Kumi na Minne (14) ya mwanzo na kuhusisha pia mazao mengine ya
Kilimo na pia kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi.
TADB
ni taasisi ya serikali ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kutatua ufinyu
mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo
nchini ambao ulikuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi
kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za
bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi;
masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo
na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya
hewa.
Afisa
Mahusiano na Masoko Mkuu wa TADB, Bw. Saidi Mkabakuli (kushoto)
akizungumza wakati Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa
William Tate Ole Nasha (MB) (mwenye tai) alipotembelea Banda la TADB.
Naibu
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB)
(mwenye tai) akizungumza na maafisa wa TADB (hawapo pichani) kuhusu
umuhimu wa Benki hiyo kuwafikia wakulima wote nchini.
Afisa
Tathmini wa Mikopo Mwandamizi wa TADB, Bw. Mubezi Buberwa (kulia) na
Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa TADB, Bw. Saidi Mkabakuli (wapili
kulia) wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB) (mwenye tai) wakati alipotembelea
Banda la TADB.
Afisa
Tathmini wa Mikopo Mwandamizi wa TADB, Bw. Mubezi Buberwa (kulia)
akifafanua hoja mbali mbali kuhusiana na mikopo inayotolewa na Benki
hiyo.
Afisa
Mahusiano na Masoko Mkuu wa TADB, Bw. Saidi Mkabakuli (kulia)
akimuelezea Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William
Tate Ole Nasha (MB) (mwenye tai) mpango wa TADB kuwafikia wakulima nchi
nzima.
EmoticonEmoticon