Mwakilishi wa UNFPA Dkt. Hashina
Begun akihutubia wakati wa kilele cha sherehe za Siku ya Wakunga
Duniani zilizofanyika kitaoifa mjini Dodoma kwenye ukumbi wa Julius K.
Nyerere ,Chuo Cha Mipango ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan akihutubia kwenye kilele cha siku ya Wakunga Duniani
ambapo Kitaifa imefanyika mjini Dodoma
Baadhi ya Wakunga wakirekodi
hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunagno wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan wakati wa kilele cha Siku ya Wangunga Duniani iliyofanyika
kwenye Ukumbi wa Julius K. Nyerere mjini Dodoma (Picha na Ofisi ya
Makamu wa Rais)
……………….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameziagiza halmashauri zote
nchini zihakikishe zinajenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa afya hasa
maeneo ya vijijini na kipaumbele kitolewe kwa wakunga ambao mara nyingi
ndio wanatoa huduma za dharura kwa wanawake wajawazito na watoto.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan ametoa agizo hilo mjini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya
Siku ya Wakunga Duniani sherehe ambazo zimehudhuriwa na Mamia ya wakunga
kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Makamu wa Rais amesema kuwa
halmashauri zikijenga nyumba karibu na vituo vya kutolewa huduma za afya
zitasaidia kupunguza matatizo ya mama na watoto wanaotaka kupata huduma
za dharura ikilinganishwa na hali ilivyo sasa ambapo baadhi ya
watumishi wa afya hasa wakunga wanakaa mbali na maeneo yao ya kazi hivyo
utoaji wa huduma za dharura kuwa duni.
Makamu wa Rais amewahimiza Wakuu
wa mikoa na wilaya kusimamia ujenzi huo kikamilifu kama
walivyoshughulikia matatizo ya madawati katika maeneo yao ili
kuhakikisha Taifa linafikia malengo yake ya kupunguza idadi ya vifo
vinavyotokana na uzazi nchini.
Kuhusu changamoto zinazoikabili
sekta ya afya nchini, Makamu wa Rais amewahakikishia wakunga na
watumishi wengine wa sekta ya afya nchini kuwa Serikali inaendelea
kufanyia kazi changamoto hizo ikiwemo uboreshaji wa maslahi kwa
watumishi wa kada hiyo pamoja na kuongeza maradufu vifaa tiba,dawa na
vitendanishi ili kuhakikisha wananchi kote nchini wanapata huduma bora
za afya.
Amesema mpaka sasa upatikanaji wa
dawa kwenye vituo vya afya nchini ni imefikia asilimia 83 hadi kufikia
mwishoni mwa Marchi 2017.
Makamu wa Rais pia amewahimiza
wakunga kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia maadili na waache tabia
ya kutoa lugha mbaya kwa wanawake wajawazito na wakunga watakaobainika
kufanya vitendo hivyo wachukuliwe hatua kali ili kukomesha tabia hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amemhakikishia
Makamu wa Rais kuwa Wizara yake itaendelea kusimamia ipasavyo utoaji
bora za afya kwa wananchi pamoja na kusimamia maadili kwa watumishi wa
sekta ya afya kote nchini.
Amesema anaimani kubwa kuwa baada
ya Serikali kuiongezea Wizara ya Afya bajeti kutoka bilioni zaidi ya 700
katika mwaka wa fedha za 2016/2017 hadi Trilioni Moja kwa mwaka wa
fedha 2017/2018 inaonyesha wazi dhamira ya dhati ya Serikali ya
kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa kiwango hali ya juu
nchini ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Kauli mbinu ya maadhimisho ya Siku ya Wakunga mwaka huu ni Wakunga,Akina mama na Familia ni washirika wa Kudumu.(Midwives,Women and Families Partners)
EmoticonEmoticon