Na Husna Saidi & Nuru Juma- MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya
Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeweka mikakati
endelevu ya kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyote vya huduma
za afya nchini.
Hayo yamebainishwa leo Bungeni
Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Adrea Kigwangalla akijibu swali
lililoulizwa na Mbunge wa viti maalum Oliver Daniel Simguruka kuhusu
hali ya upatikanaji wa dawa nchini katika kikao cha saba cha Bunge.
Dkt. Kigwangalla alisema kuwa hali
ya upatikanaji wa dawa nchini umeimarika kwa asilimia 83 hivyo kufanya
huduma hiyo ya afya kuwa bora.
“Hadi kufikia Aprili 2017 jumla ya
shilingi bil.112 mil.198, 920,456 zimeshatolewa na kupelekwa kwenye
bohari ya dawa ili kuwezesha vituo vya huduma za afya vya umma kupata
mahitaji ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi”, alisema Dkt. Kigwangalla.
Aidha, alisema ongezeko hilo la
fedha limesaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya
afya tofauti na miaka iliyopita.
Aliongeza kuwa hadi kufikia
Januari 15 mwaka huu Mkoa wa Kagera pekee ulipokea kiasi cha shilingi
bil.4 mil.150, 767,216 kupitia fungu namba 52 kutoka kwa Wizara hiyo ili
kuboresha huduma ya afya Mkoani humo.
Akizungumzia ujenzi wa bohari za
dawa katika kila kanda Dkt. Kigwangalla alisema kuwa Serikali imeendelea
kuitatua changamoto hiyo baada ya hapo awali kukabiliwa na changamoto
ya fedha katika kujenga bohari za dawa kila kanda.
Kwa upande mwingine aliwaomba
viongozi wa ngazi zote waweze kushirikiana katika kudhibiti wizi wa dawa
katika vituo vya huduma za afya kwa sababu hili ni jukumu la kila mmoja
na pia alitoa wito kwa wananchi kuweza kutoa taarifa za wizi wa dawa
ili sheria iweze kuchukuliwa.
EmoticonEmoticon