Katika kuhakikisha Mkoa wa Rukwa
Upo salama kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola yatakayoweza
kujitokeza, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote
Stephen amefanya ziara ya siku tatu katika mwambao wa ziwa Tanyangika
kwenye Kata ya Kirando, Kabwe na Kasanga vijiji ambavyo vipo jirani na
nchi ya DRC ili kujionea namna Halmashauri ya Nkasi na Kalambo
zilivyojipanga kuhakikisha kuwa ugonjwa huo hautii mguu katika Mkoa na
nchi kwa ujumla.
Ziara hiyo aliianza siku ya
Ijumaa tarehe 26 hadi 28. 05. 2017 mara baada ya kumaliza kumalizika kwa
mafunzo ya siku tatu yaliyohusu utumaji wa taarifa za magonjwa kwa
kieletroniki (e-idsr) yenye kusisitiza tahadhari ya ugonjwa wa ebola
uliopo katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
yaliyotolewa kwa wahudumu wa afya wa Serikali na Sekta binafsi kwa
Halmashauri mbili za Manispaa ya Sumbawanga na Sumbawanga vijijini.
Mafunzo ya awamu ya pili
yanatarajiwa kumalizika tarehe 31. 05. 2017 kwa Halmashauri za Kalambo
na Nkasi ikiwa ni muendelezo wa awamu ya kwanza kwa Halmashauri ya
Sumbawanga Vijijini na Manispaa ya Sumbawanga yaliyoisha tarehe 26.
Mwezi wa tano.
Ili kujiridhisha na maandalizi ya
Halmashauri zinazopakana na nchi za jirani yaani Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na Zambia Mkuu wa Mkoa alipita katika
bandari maarufu za pwani ya ziwa Tanganyika na kuongea na vyombo vya
usalama ikiwemo uhamiaji, Sumatra, TRA, jeshi la polisi, jeshi la
wananchi, maafisa forodha pamoja na maafisa afya kutoka Wilayani.
Pia Mh. Zelote aliongea na
viongozi wa serikali za vijiji na kata wakiwemo madiwani, watendaji wa
kata na vijiji, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, maafisa ugani wa kata
na vijiji, maafisa afya wa kata na vijiji na kufanya mikutano ya hadhara
ili kuwapa wananchi ujumbe aliokwenda nao katika kuhakikisha ugonjwa
huo haunusi katika mkoa wa Rukwa na nchi ya Tanzania.
Pamoja nae Mheshimiwa Mkuu wa
Mkoa aliambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Boniface Kasululu, Mratibu
wa Chanjo Mkoa Gwakisa Pamoja na Afisa kutoka Wizara ya Afya wa
usimamizi na ufuatiliaji Solomon Mushi, Mkuu wa Wilaya, makatibu tawala
wa wilaya pamoja na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya.
Katika kila Wilaya aliyopita Mh.
Zelote alihakikisha anapewa taarifa za maandalizi ya Wilaya na kisha
kwenda kwenye mipaka ili kujionea kwa macho yake maandalizi hayo na pia
kuongea na wananchi wanoishi karibu na mipaka hiyo.
Wakati akiwa kwenye ziara hiyo
Mh. Zelote alikuwa akisisitiza utayari pamoja na kujihadhari kwa
viongozi wa serikali za vijiji na kata na pia kwa vyombo vya usalama vya
maeneo hayo ya mipakani.
Katika suala la utayari Mh.
Zelote Alisema kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa juu ya athari ya
ugonjwa huo na namna ya kujikinga nao ikiwa ni pamoja na kuelezwa dalili
za ugonjwa na njia za maambukizi ya ugonjwa huo na kuwasisitiza
wananchi kwenda zahanati pindi wanapojiskia kuumwa na sio kukimbilia
kwenye maduka ya dawa na kuagiza vidonge bila ya kujua ugonjwa
anaoutibu.
Pia katika kusisitiza hilo Mh.
Zelote aliwasihi wananchi kutokimbilia kwa waganga wa kienyeji pindi
wanapoumwa na badala yake wakimbilie kwa wataalamu wa afya kwenye
zahanati ama vituo vya afya. Na kuwaonya kuwa kupitia hizi taarifa za
ugonjwa wa ebola kunaweza kukajitokeza matapeli ambao watajitangaza
kuutibu ugonjwa huo jambo ambalo si kweli, hivyo aliweka msisitizo kuwa
ugonjwa wa Ebola hauna Tiba.
“Mtu yeyote atakayejiskia vibaya
basi haraka akimbilie kwenye zahanati ama kituo cha afya na sio kwa
mganga wa kienyeji, na mjiepushe mbali sana na matapeli wanaotibu watu
vichochoroni ama wanaosema dawa ya Ebola ipo,…. Hakuna,” Mh. Zelote
alieleza.
Pamoja na hayo Mh. Zelote alionya
kuwa katika kusimamia jambo hilo hatakuwa na utani, dhihaka ama
masihara kwayeyote atakaekiuka taratibu zilizowekwa ili kujihadhari na
ugonjwa huo kuingia katika mkoa wa Rukwa.
“Mimi nafahamu kwamba watu
wanaoishi humu kwenye mipaka wameoa ama kuolewa katika nchi za jirani,
na kwamba watanzania utamaduni wetu ni ukarimu kwa wageni lakini katika
hili tupunguze ukarimu mpaka jambo hili liishe, na yeyote
atakayegundulika anamhifadhi mgeni kinyume na taratibu, huyo ni
mhalifu,” Mkuu w Mkoa alisema.
Katika kuonesha athari kubwa
inayoweza kupatikana endapo uginjwa huo utapenya katika nchi yetu Mh.
Zelote alieleza kuwa gharama za kumshughulikia mgonjwa mmoja ni kubwa
sana na kuongeza kuwa endapo ugonjwa huo unathibitishwa kwenye nchi
Fulani basi tatizo hilo si la nchi hiyo tu ni la dunia nzima.
“Nguo inayotumika kumshughulikia
mtu mmoja inauzwa milioni 10 na kwa wenzetu huko afrika ya magharibi
Ivory Coast ambako walikumbana nao watu 11,000 walifariki, wakiwemo
madaktari ambao walikuwa wakiwauguza wagonjwa, mtu mmoja tu akiupata
basi kijiji kizima kinafungwa hakuna mtu kuingia katika kijiji hicho
wala kutoka,” Mh. Zelote alisisitiza.
Lakini pia aliwatoa hofu wananchi na kuwaambia kuwa mpaka sasa Tanzania hakuna mgonjwa hata mmoja wa Ebola.
Nae Daktari wa Mkoa Dkt. Kasululu
alisema kuwa tangu ugonjwa huo kutolewa taarifa na Wizara ya Afya
tarehe 12. 05. 2017 watu watatu wlikuwa wamefariki na wengine 12
walikuwa wako chini ya uangalizi lakini hadi kufuikia tarehe 25. 05.
2017 idadi ya wagonjwa iliongezeka hadi kufikia wagonjwa 45 na kuongeza
kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka kadiri siku zinavyokwenda mbele.
“Idadi ya wagonjwa imekuwa
ikiongezeak kila kukicha hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunajiandaa na
kujihadhari kweli, maana wagonjwa hawa wapo kwenye misitu ambapo
usafiri wa kawaida haufiki isipokuwa Helkopta na pikipiki, hivyo
wagonjwa wanaweza kuwa wengi na bado hawajajulikana,” Dkt Kasululu
alisisiza.
Nae Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya
ya Nkasi Dk. Makundi Maige alielezea mikakakti ya Halmashauri ya Nkasi
namna ilivyojipaga kuhakikisha wanakaa mbali na ugonjwa hatari wa Ebola.
“ Wilaya imeainisha kata tatu za
Kirando, Kabwe na Wampembe ambazo zimetengwa kwaajili ya kupokea wageni
kutoka nchi za jirani, tukifahamu kuwa katika mwambao wa Ziwa Tanganyia
kuna Kata 10 ambazo ugonjwa huu unaweza kuingia kwa urahisi, ambazo ni
Kabwe, Kirando, Wampembe, Itete, Kipili, Mkinga, Korongwe, Ninde,
Kizumbi na Kala,” Dk. Makundi aliainisha.
Katika kubainisha upokezi wa
wageni hao Dk. Makundi alisema kuwa kituo cha Wampembe kitapokea wageni
wanoelekea kijiji cha Kilambo hadi Msamba, Kituo cha Kirando kitapokea
wageni wanaoelekea kijiji cha Ninde hadi Kazovu na kituo cha Kabwe
kitapokea wageni wanaoelekea kijiji cha Utinta hadi Kalila.
Na kuongeza kuwa wageni wote
kutoka nchi za jirani watalazimika kupitia katika vituo hivyo na sio
kuingia kiholela kama ilivyozoeleka na kabla ya kuendelea na safari zao
watakuwa wakichunguzwa afya zao.
Kwa kuzingatia namna ugonjwa huo
unavyoenea Wilaya imetenga eneo maalum kwaajili ya matibabu ili kuepuka
kuchanganya wagonjwa watakaobainika kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola.
Pamoja na hayo Wilaya imejipaga
kuzizungukia kata zote 10 na kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wa
maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha viongozi wa dini, wazee
maarufu, vijana, waalimu na wanafunzi juu ya ugonjwa huo hatari.
Nao upande wa Wilaya ya Kalambo
walieleza mipango yao juu ya udhubiti wa ugonjwa huu, ambapo mganga Mkuu
wa Wilaya Dkt. Alcado mwamba aliweza uainisha tahadhari mbalimbali
ambazo Wilaya imezichukua kuhakikisha wanaudhibiti ugonjwa huo
kutokuingia katika Wilaya hiyo.
Miongoni mwa tahadhari
walizochukua ikiwa ni kuwasambazia wananchi vipeperushi vyenye kutoa
elimu ya ugonjwa wa Ebola lakini pia kuihamasisha jamii kutoa taarifa
haraka kwa uongozi wa serikali pindi tu wakibaini kuna mgeni aliyeingia
kinyume na taratibu zilizowekwa.
EmoticonEmoticon