Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) uliofika
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kubadilishana nao mawazo. Kulia ya
Balozi Seif ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Bwana Kajubi
Mukajanga na Kushoto ya Balozi ni Mkuu wa Ofisi ya Baraza la Habari
Tanzania (MCT) upande wa Zanzibar Bibi Shifaa Hassan .
Mkuu
wa Ofisi ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) upande wa Zanzibar Bibi
Shifaa Hassan akifafanua jambo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif walipokutana nae kwa mazungumzo.
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Bwana Kajubi Mukajanga Kulia ya Balozi
Seif akielezea mikakati ya Baraza la Habari Tanzania inavyofanya kazi
Zanzibar katika kuhakikisha Maadili ya Habari yanazingatiwa na Wana
Habari wote Nchini.
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Bwana Kajubi Mukajanga akimkabidhi Balozi
Seif Vitabu mbali mbali vilivyochapishwa na Baraza hilo kuhusu Tasnia ya
Habari Tanzania.
Balozi
Seif akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa juu wa Baraza la Habari
Tanzania mara baada ya kubadilishana mawazo Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar. Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari
Bwana Kajubi Mukajanga na Muandishi wa Makala wa MCT Yussuf Mpinga.
Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Ofisi ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) upande
wa Zanzibar Bibi Shifaa Hassan, Muhariri wa Machapisho wa MCT Khamis
Mzee na Mkuu wa Kitengo cha Rasilmali Watu cha MCT Bivi Ziada Kilobo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inasubiri kuyapokea kwa ajili ya kuyafanyia kazi
mapendekezo yatakayowasilishwa ya Rasimu ya Sera ya Habari Zanzibar
katika kuona Sekta ya Habari Nchini inakuwa imara.
Alisema
Taasisi zinazohusika na jukumu la kusimamia masuala hayo ni vyema
zikahakikisha kwamba zinaharakisha mapendekezo hayo ili ile dhana ya
Uhuru wa kupata Habari bila ya kuogopa inapatikana.
Balozi
Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa
Baraza la Habari Tanzania { MCT } ulioongozwa na Katibu Mtendaji wake
Bwana Kajubi Mukajanga aliokutana nao hapo Afisini kwake Mtaa wa Vuga
Mjini Zanzibar.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kutoa kila aina ya msaada
katika kuona Sekta hiyo muhimu kwa jamii inawajibika ipasavyo katika
kuwapasha Habari Wananchi.
“
Habari ni Sekta muhimu inayotoa Taarifa na Elimu na kuwahusisha moja kwa
moja Wananchi wa kawaida wakiwemo wakulima Vijijini ”. Alisema Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi
Seif kupitia Uongozi wa Baraza hilo la Habari Tanzania aliwakumbusha
Wana Habari kuzingatia sheria na Maadili yao ya kazi katika kuandika
Habari wanazozifanyia Utafiti wa kina ili zisaidie Wananchi kupata
Habari za ukweli.
Akizungumzia
changamoto ya Vitambulisho vya Kazi inayowakumba Wana Habari wanaotokea
Tanzania Bara na kupangiwa kufanya kazi Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar aliahidi kulifuatilia kwa kina suala hilo ambalo bado
halijawa kero kama yalivyo masuala mengine katika utendaji.
Alisema
Waandishi wa Habari wanaotokea Tanzania Bara wanapaswa kuandaliwa
utaratibu maalum wa kupata vibali vya kazi kwa vile wao hawahusiani na
kuwa na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi katika kuomba kibali cha
kufanya Kazi Zanzibar.
Balozi
Seif alieleza kwamba mfumo unaotumika katika kuwapasha Habari Wananchi
wa pande zote za Muungano hauna mipaka licha ya kwamba Sekta ya Habari
sio Taasisi iliyomo ndani ya masuala ya Muungano.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Baraza la Habari
Tanzania { MCT } kwa umakini wake wa kusimamia Sekta ya Habari Nchini
Tanzania.
Mapema Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Bwana
Kajubi Kukajanga alisema Kamati ya Maadili ya Bahara la Habari Tanzania
imekuwa na utaratibu wa kufanya ziara za kusikiliza malalamiko
yanayotolewa na Wananchi wanaoandikwa visivyostahiki katika Vyombo mbali
mbali vya Habari.
Bwana
Kajubi alisema Wajumbe wa Kamati hiyo kupitia ziara hizo hupata fursa za
kushauri, kuelekeza pamoja na kuwaonya na wengine kuwachukuliwa hatua
za kisheria Wana Habari wanaofanya makosa katika kuandika Habari chafu
dhidi ya wananchi mbali mbali.
Alisema
Viongozi hao pia wanajaribu kusaidia Wana Habari wanaotoka Tanzania
Bara kuondokana na ukakasi wa kupata Vitambulisho vitakavyowapa fursa ya
kufanyakazi kwa upana zaidi bila ya vikwazo.
Naye Mkuu wa Ofisi ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) upande
wa Zanzibar Bibi Shifaa Hassan alisema Mchakato wa Sera ya Habari
Zanzibar umeanza tokea mwaka 2010 kwa mashirikiano baina ya Idara ya
Habari Maelezo, Tume ya Utangazaji Zanzibar pamoja na baadhi ya Viongozi
wa Taasisi za Serikali.
Bibi
Shifaa alisema Zanzibar imekuwa tajiri katika masuala ya Historia ya
Habari kutokana na kuanza mapema kwa Sekta hiyo ndani ya Ukanda mzima wa
Afrika ya Mashariki.
Alisema
Ofisi ya Baraza la Habari Tanzania upande wa Zanzibar ilianzishwa mwaka
2003 na kuanza na Mpango Maalum wa harakati za kutoa mafunzo kwa Wana
Habari wachanga wa vyombo mbali mbali vya Habari wakiwemo pia wale
waliomaliza masomo yao ya sekondari walioamua kujiunga na Tasnia hiyo.
Bibi
Shifaa alieleza kwamba mpango huo ulikwenda sambamba na kutoa machapisho
ya vitabu mbali mbali, kufanya utafiti kuhusu shirika la Habari
Zanzibar mambo yaliyoibua kupatikana kwa Kitabu cha Historia ya masuala
ya Habari Zanzibar kilichozinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mwaka ulipita.
Viongozi
wa Baraza la Habari Tanzania tayari wapo Visiwani Zanzibar kuhudhuria
maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani inayofikia kilele chake
ifikapo Tarehe 3 Mei ya kila mwaka ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/5/2017.
EmoticonEmoticon