Na Othman Khamis Ame, OMPR
Kamati
ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi imekutana
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kutathmini Mvua za Masika na muelekeo
wa kukabiliana na changamoto zilizoanza kuibuka.
Tathmini
hiyo imekuja kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Maeneo
mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba na kuathiri Nyumba 325 Mkoa
Kusinin Pemba, Nyumba 667 kuhamwa ndani ya Mkoa Mjini Magharibi pamoja
na kubomoka kwa miundombinu ya Bara bara na baadhi ya Madaraja hasa
Kisiwani Pemba.
Akitoa
Taarifa za awali za athari ya mvua zilizojitokeza kwa mwaka wa 2017
tokea kuanza kwa msimu wa Mvua za Masika, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema athari ya Mvua
hizo zimesababisha maporomoko ya ardhi yaliyosababisha kufukia kwa
baadhi ya Nyumba na Bara bara.
Nd.
Ali alisema ziara za Viongozi wa Serikali zimegundua athari kubwa ya
uharibifu wa miundombinu ya Bara bara na nyumba kutokana na mvua hizo
hasa katika Mkoa wa Kusini Pemba na kusababisha kifo cha Mtoto Mmoja
Ramadhan Mohamed baada ya kuangukiwa na ukuta wa Madrasa Chanjani Chake
Chake Pemba.
Naye
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar Nd.
Mohamed Khamis Ngwali alisema bado Visiwa vya Unguja na Pemba viko
katika msimu wa mvua hali ambayo wananchi wanapaswa kufuatilia Taarifa
zainazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Nd.Ngwali
alisema viwango vya mvua katika visiwa vya Zanzibar viongezeka kama
vilivyotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania mnamo Tarehe 28
Mwezi uliopita na kuanza kunyesha mara moja siku iliyofuata.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Idara ya Kinga Wizara ya Afya Dr.Fadhil Abdulla
alieleza kwamba Wizara ya Afya tayari imeshajiandaa na changamoto
yoyote inayoweza kujitokeza endapo kutaibuka kwa maradhi ya mripuko
katika kipindi hichi cha msimu wa mvua za masika.
Dr.
Fadhil alisema udhibiti wa vyakula vinavyouzwa katika maeneo ya wazi
bado mgumu na ndio uliochangia kuibuka kwa maradhi ya Kipindupindu mwaka
jana kwa asilimia 16%.
Alisema
katika kukabidhiana na udhibiti wa mfumko wa maradhi ya kuambukiza
Wataalamu wa Afya tayari wameshapima wagonjwa 22 walioonyesha ishara ya
kusumbuliwa na maradhi ya matumbo ya kuharisha.
Akiahirisha
Kikao hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema ipo haja ya kuandaliwa mikakati ya muda mrefu ya kukabiliana na
changamoto zinazojitokeza kila mwaka wakati wa msimu wa mvua za Masika.

EmoticonEmoticon