Taifa
Stars ya Tanzania kesho Machi 28, 2017 saa 10:00 jioni inaingia tena
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kucheza na Intamba Murugamba ya Burundi
katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kwa mujibu wa kalenda ya wiki ya
mechi za kimataifa ya FIFA.
Huu ni mchezo wa pili kwa Taifa
Stars kucheza ndani ya wiki moja baada ya ule wa awali dhidi ya The
Zebras ‘Pundamilia’ wa Botswana uliofanyika Uwanja huo wa Taifa, jijini
Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Katika mchezo huo wa Jumamosi,
Taifa Stars ambayo kwa sasa inanolewa na Salum Mayanga akisaidiwa na
Patrick Mwangata ambao ni makocha wapya wa kikosi hicho, walishinda kwa
mabao 2-0.
Tayari Intamba Murugamba wametua
nchini tangu jana Jumapili saa 4.30 asubuhi na kufikia Hoteli ya De Mag
iliyoko, Kinondoni, Dar es Salaam na jioni yake walifanya mazoezi kwenye
Uwanja wa Karume, Ilala jijini. Leo Jumatatu, inafanya mazoezi Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Ndani ya kikosi hicho wamo
washambuliaji wawili wanaotamba katika klabu za Simba na Young African
za Dar es Salaam. Nyota hao ni Amisi Tambwe wa Young Africans na Laudit
Mavugo wa Simba.
Leo Jumatatu Machi 27, 2017 saa
8.30 alasiri nyota hao wakiongozana na kocha wao watazungumza na
wanahabari namna walivyoajiandaa kucheza na Taifa Stars ambayo pia ina
nyota wengi wanaocheza na wachezaji hao wa Burundi katika klabu za Simba
na Young Africans.
Wakati Mavugo ni mshambuluaji,
anatarajiwa kuwa na wakati mgumu mbele ya walinzi mahiri ambao pia wako
Simba kama vile Abdi Banda na Mohammed Hussein wakati Andrew Vicent
anayetoka Young African atakuwa kisiki kwa Tambwe wanayecheza naye timu
moja kama makocha watawapanga.
Kwa upande wake, Mayanga
alifurahishwa na ushindi wa Jumamosi iliyopita dhidi ya The Zebras ya
Botswana na hivyo amehimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi katika
mchezo wa kesho.
Katika kuunga mkono wito wa Kocha
Mayanga, TFF imebakiza viingilio vya mchezo huo kuwa sawa na vile vya
Jumamosi iliyopita kwani katika mzunguko ambao unachukua mashabiki wengi
kiingilio kitakuwa ni Sh 3,000.
Kwa upande wa VIP “A” Kiingilio
kitakuwa ni Sh 15,000 wakati VIP “B” na VIP “C” kiingilio kitakuwa ni Sh
10,000. Viingilio hivyo vimelenga kuwaalika Watanzania wengine kwenda
uwanjani.
EmoticonEmoticon