Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati), akielekea kukagua Bandari
ya Kemondo mkoani Kagera ili kujionea utendaji kazi wake. Kulia ni
Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo.
Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa,
Bw. Abel Moyo, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa (Wa pili kushoto), njia ya reli katika bandari ya
Kemondo mkoani Kagera, ambayo itaruhusu mizigo itakayokuja kwenye
mabehewa kwa njia ya meli iweze kupakuliwa na kupelekwa kuhifadhiwa
kwenye maghala.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akikagua sehemu ya maegesho ya meli
katika Bandari ya Kemondo, mkoani Kagera. Bandari hiyo ina upana wa mita
100.
Muonekano wa gati ya meli katika Bandari ya Kemondo, mkoani Kagera.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA), mkoani Kagera Eng. Zephrine Bahyona, akifafanua jambo
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
(wa nne kulia), alipokuwa akikagua Kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa
huduma katika mto Kyanyabasa, mkoani Kagera.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja
wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani Kagera Eng. Zephrine
Bahyona, alipotembelea na kukagua kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa
huduma katika mto Kyanyabasa, mkoani Kagera.
Muonekeano wa kivuko cha
Kyanyabasa kinachotoa huduma katika mto Kyanyabasa, mkoani Kagera.
Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba watu sitini au magari mawili madogo
kwa wakati mmoja.
………………..
Imeelezwa kuwa kukamilika kwa
ukarabati wa meli ya MV Umoja kutarudisha huduma ya usafirishaji wa
mizigo katika kanda ya ziwa kupitia bandari ya Kemondo iliyopo mkoani
Kagera.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati
akikagua Bandari hiyo kuangalia maendeleo yake, na kuitaka Mamlaka ya
Bandari Nchini (TPA), Shirika la Reli Nchini (TRL), na Kampuni ya Huduma
za Meli (MSCL), kuanza kuandaa Mfumo mmoja wa kutoa Stakabadhi ili
kuwarahisishia wateja wake huduma za usafirishaji wa mizigo.
Aidha, Waziri Mbarawa ameitaka TRL
kukarabati njia za reli bandarini hapo haraka iwezekanavyo ili kuruhusu
mizigo itakayokuja ikiwa kwenye mabehewa kwa njia ya meli iweze
kupakuliwa pindi Meli hiyo itaposhusha.
“Serikali imefanya ukarabati wa
meli ya MV Umoja ambayo itabeba mizigo ikiwa kwenye mabehewa na reli hii
inahitaji ukarabati mapema ipasavyo nawaagiza TRL kufanya ukarabati wa
reli ili kusiwepo usumbufu wowote wakati wa kushusha na kupakia mizigo
hiyo” , amesema Profesa Mbarawa.
Ameiagiza Mamlaka hiyo kuanza
kutafuta tena wateja ambao kwa muda mrefu walikuwa wamepotea kutokana
na bandari hiyo kusuasua kutoa huduma zake kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Meneja wa TPA
Kanda ya Ziwa Bw. Abel Moyo, amemuahidi Waziri huyo kutekeleza agizo
lake kwa kushirikiana na TRL pamoja na MSCL na kuwahakikishia
wafanyabiashara wa kanda ya ziwa kuwa na matumaini mpya ya kupata
usafiri bora na wa uhakika.
Katika hatua nyengine, Waziri
Mbarawa ametembelea na kukagua Kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa huduma
katika mto Kyanyabasa na kumtaka Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na
Umeme (TEMESA) mkoani humo, Eng. Zephrine Bahyona, kutoa huduma bora
sambamba na kukusanya mapato ili kuweza kutatua changamoto ndogondogo
zinazowakabili.
Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani humo Eng. Zephrine Bahyona, amezitaja
baadhi ya changamoto zinazoathiri utendaji mzuri wa kivuko hicho kuwa ni
kukatika kwa magugu maji na hivyo kupelekea kusombwa kwa kivuko.
Waziri Profesa Mbarawa pia
amekagua barabara ya Uyovu- Bwanga yenye urefu wa kilometa 45 mkoani
Geita na kuridhishwa na kasi ya Mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo
ambapo ujenzi wake kwa sasa umefika asilimia 56.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WIzara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
EmoticonEmoticon