DC KOROGWE AONGOZA OPERESHENI YA KUHARIBU MASHAMBA YA BANGI KUUNGA JITIHADA ZA SERIKALI KUPAMBANA NA MATUMZI YA DAWA ZA KULEVYA

March 15, 2017
  Mkuu wa wilaya ya korogwe,Mhandisi Robart Gabriel kushoto akizungumza na askari katika msitu wa kijiji cha Kijungumoto kata ya Mashewa kabla ya kuanza zoezi la uteketezaji wa mashamba ya bangi wilayani Korogwe



 Ofisa Upelelezi Mkoani wa Tanga,Amedeus Tesha akishiriki uvunaji bangi.
 Mkuu wa wilaya ya korogwe,Mhandisi Robart Gabriel akishiriki uvunaji wa bangi.


 DC Korogwe,Robart akizungumza na askari wa jeshi la polisi ambao wameshiriki zoezi hilo.
 Bangi ambayo imeshavunwa.
 Baadhi ya askari wa FFU tanga wakiwa wamepumzika baada ya zoezi la uvunaji.

 Mkuu wa wilaya ya korogwe,mhandisi Robart akichoma bangi baada ya kuivuna.
Pichani mkono wa kulia ni mkuu wa wilaya korogwe,Robart akiongea na viongozi wa kijiji cha kijungumoto kushoto.

NA SOPHIA WAKATI,KOROGWE
EKARI 25 za mashamba ya bangi zimefyekwa huku zikiteketezwa kwa moto katika kitongoji cha Nembwibwi,kijiji cha Kijungumoto kata ya Mashewa iliyopo wilayani Korogwe hatua ambayo imeelezwa kuwa ni mkakati wa serikali katika kutokomeza madawa ya kulevya ili kuokoa nguvu kazi.

Operesheni ya kuharibu mashamba hayo imeongozwa na mkuu wa wilaya ya Korogwe Robert Gabriel ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Usalama wilayani humo akiwa ameshirikiana na maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama,askari polisi,magereza na wale wa kutoka uhamiaji.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya Mhandisi Robert Gabriel ni kwamba taarifa za uwepo wa mashamba hayo alizipata kupitia kwa wasamaria wema na ndipo uchunguzi ukafanyika hatua iliyowezesha operesheni kufanyika kwa siku mbili mfululizo huku wahusika na bangi wakisakwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Korogwe mkuu huyo wa wilaya alisema,Korogwe bila uwepo wa madawa ya kulevya inawezekana na kwamba operesheni hiyo ambayo imeanza itakuwa endelevu lengo likiwa kupiga marufuku kabisa uwepo wa bangi na bidhaa nyingine haramu.

Pamoja na hayo,mkuu huyo wa wilaya alielezea kusikitishwa kwake na viongozi wa serikali za vijiji hasa wevyeviti na watendaji kutokuonyesha ushirikiano madhubuti katika kufanikisha vita hivyo dhidi ya madawa ya kulevya ambapo alisema kuanzia sasa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Gabriel alisema,inashangaza kuona kwamba bangi imekuwa ikilimwa kwa wingi tena kwa muda mrefu kwenye baadhi ya maeneo huku viongozi hao wakidai kukosa taarifa juu ya uwepo wa mashamba hayo mazingira ambayo yanatia wasiwasi juu ya uadilifu wao na kwamba wakati wa wao kubadilika umefika.

"Hii haitawezekana,kuanzia sasa kiongozi ambaye atashindwa kutoa taarifa kama eneo lake kuna shamba la bangi ama kuna jambo lolote haramu linaendelea tutamchukulia hatua kali za kisheria,hivi inawezekanaje kiongozi ndani ya eneo lake la utawala hajui kinachoendelea"alihoji DC.

Uamuzi huo wa DC Gabriel kuwashughulikia kisheria viongozi wa vijiji umekuja baada ya kuomba kutajiwa wahusika wa mashamba ya zao la Bangi huko kitongoji cha Nembwibwi ambapo kila kiongozi aliyemuuliza alidai kuwa hakuwa akifahamu kama kulikuwa na kilimo hicho cha bangi.

Kaimu afisa mtendaji wa kata ya Mashewa Hamisi Shekigeda alipoulizwa na mkuu wa wilaya Robert Gabriel kama anafahamu kwenye eneo lake la kazi kulikuwa na mashamba ya bangi alijibu kwamba hakuwa akijua lolote hadi pale alipofika kwenye eneo hilo alikoitwa akielezwa operesheni inafanyika.

Alitanabaisha kuwa yeye (Shekigenda) hakuwa akifika kwenye eneo hilo kwa vile lilikosa kufahamika ni nani hasa mmiliki wake halali kutokana na kuwepo kwa mgogoro kati yao watu wa Korogwe na Lushoto huku kila upande ukidai kuwa na haki ya kulimiliki eneo hilo la ardhi.

Naye mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kijungumoto Katuni Ally alimueleza DC Robert Gabriel kuwa hakuwa akifahamu iwapo eneo hilo kunaendeshwa kilimo cha zao haramu la Bangi ambapo aliahidi kuendelea kushirikiana na serikali kwa karibu ili kutokomeza kilimo hicho cha zao hilo.

Licha ya ahadi hizo DC Robert Gabriel aliahidi kufanya ufuatiliaji wa karibu kukomesha vitendo vyote haramu wilayani mwake huku akisistiza kuwa ushirikiano unahitaji kwa wadau wote hatua ambayo itaweza kuliokoa Taifa huku akisistiza kusema kuwa Korogwe bila ya dawa za kulevya inawezekana.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »