MPIGA CHAPA MKUU ASISITIZA KAMPUNI KUENDELEA KUJISAJILI

March 25, 2017
Mpigachapa Mkuu  wa Serikali,Cassian Chibogoyo akionesha waandishi wahabari (hawapo pichani) katika moja ya mikutano yake  rangi sahihi  ya bendera yaTaifa, kulia ni Afisa Habari wa Idara Habari Maelezo, Frank Shija. (NA MPIGA PICHA WETU)

Leonce Zimbandu

MPIGACHAPA Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo ameendelea kusisiti za na kuzitaka taasisi za serikali, binafsi za uchapishaji  kuendelea kujisajili katika ofisi hiyo na kuepuka usumbufu wa kubainika kwenye msako.

Kauli hiyo imetolewa baada ya kutoridhishwa na kasi ya kampuni za uchapishaji zilizojitokeza tangu wito huo utolewe Februari 13, mwaka huu, kampuni 24 tayari zimejitokeza.

Chibogoyo  aliyasema hayo alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam leo  wakati akijibu swali kuhusu kampuni za uchapishaji zilizotii sharia kujisajili  bila shuruti.

Alisema amesikitishwa na mwitikio mdogo wa usajili wa kampuni na taasisi za uchapishaji, hivyo akiwa muungwana ameamua kutumia fursa ya  kuwakumbusha  watimize wajibu wao kisheria.

“Inawezekana katika mkutano wangu  sikueleweka vizuri lakini usajili unahusu kampuni binafsi na serikali kwa lengo la  kutambua shughuli zao na kuepuka kujificha,” alisema.

Alisema baada ya muda uliotolewa kukamilika na ofisi hiyo ikapata  taarifa kuwa ipo taasisi au kampuni inajihusisha na uchapishaji, Ofisi itachukua hatua ya kuifuatilia.

Hivyo kabla ya hali hiyo ya ufuataliaji, itakuwa busara kwa wachapishaji hao kujisajili  ndani ya siku tano zilizobaki tangu wito huo ulipotolewa. 

Aidha, alisema   ili kuondoa usumbufu kwa kampuni za uchapishaji za mikoani, zinaweza kujisajili kwa kupitia mtandao wa Ofisi ya Mpigachapa.

Alisema Wachapishaji   halali watakaojiorodhesha watakaribishwa na kupewa fursa ya kutoa mawazo ya kuiweka nchi mahali salama kupitia nyaraka.

Hatua hiyo imechukuliwa  ili kuendeleza vita dhidi ya wachapishaji wa nyaraka bandia kwa kuwasaka nyumba kwa nyumba, iwapo watashindwa kujitokeza na kujisajili kwa hiari.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »