Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisisitiza jambo mara baada ya kutembelea Shamba litakaloandaliwa kwa ajili ya Maonesho ya Nanenane lililopo Mkoani Morogoro
Na Mathias Canal, Morogoro
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amefanya ukaguzi wa eneo kwa ajili ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) ili kujiridhisha na kutoa maelekezo ya maandalizi kwa kufyeka majani yaliyopo katika eneo la JKT Mtaa wa Nanenane ikiwa ni hatua za ufanisi kwa ajili ya kuelekea Maonesho ya Nane Nane mwanzoni kwa mwezi Agosti.
Kayombo amesema kuwa lengo kuu la kuzuru kwanza ilikuwa ni kujionea eneo hilo sambamba na kuona hali ya utendaji kazi ili kuanza ufyekaji na kuanza kulima mazao ambayo yanakusudiwa kuoneshwa na Manispaa ya Ubungo.
Amesema kuwa katika utendaji wake amekusudia kwenda mwenyewe Field ili kuona hali ya utendaji ilivyo sio kupelekewa Taarifa pekee kwani kufanya hivyo Ukurugenzi alionao utakuwa hauna maana kama ataishia ofisini.
"Rais ametupa mamlaka makubwa ya kuwatumikia wananchi sasa kama tunakaa ofisi pekee nchi haiwezi kusonga mbele badala yake ili tuweze kuwa na mafanikio katika utendaji pamoja na Kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali ni wazi kwamba tunapaswa kuzuru katika maeneo yote tunayoyaongoza" Alisema Kayombo
MD Kayombo amewapa maelekezo Afisa Kilimo na Afisa Mifugo na Uvuvi kuanza haraka iwezekanavyo usafishaji wa shamba hilo lenye ukubwa wa Mita za Mraba 3600 ili kulima na kupanda mazao kusudiwa kwa ajili ya Maonesho ya Kilimo Nane Nane.
Maelekezo mengine ni pamoja na kununua viuatilifu kwa ajili ya kuua wadudu waharibifu na magonjwa, kuandaa mabango na kuainisha aina mbalimbali za malisho iliyooteshwa na kujenga bwawa la samaki.
Kayombo alisema kuwa eneo hilo limenunuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa ajili ya Maonesho ya Nane Nane ambayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha wakulima, Wafugaji na wavuvi kwa kuwaelimisha na kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia na mbinu za kuongeza uzalishaji katika eneo la Uvuvi, Kilimo na Ufugaji.
Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Kaimu Afisa Kilimo wa Manispaa ya hiyo Ndg Salim Msuya amesema kuwa wanataraji kuanza kutekeleza hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kujenga mabanda ya mifugo na sehemu za kusindika mazao ya mifugo, kuandaa mavazi rasmi kwa ajili ya washiriki wa Maonesho.
Mengine ni kukusanya bidhaa za mazao mbalimbali ya wafugaji, wakulima na wavuvi watakaoshiriki Maonesho hayo ya Kilimo Nane Nane kwa ajili ya kuyapeleka Morogoro.
Sambamba na hayo pia Msuya amesema kuwa maandalizi mengine itakuwa ni kutengeneza matuta ya kuoteshea malisho, Kununua mbolea na kuweka kwenye eneo la malisho ya mifugo, kufunga maji katika eneo la malisho yatakayotumika kwa ajili ya umwagiliaji na mifugo itakayopelekwa wakati wa Maonesho.
Msuya ameeleza kuwa maandalizi mengine itakuwa ni kuandaa mashimo katika matuta ya kuotesha miche, Vipande na Mbegu za malisho pamoja na kutayarisha eneo la kwa kusafisha eneolima na kufanya Layout ya eneo la kuchimba bwawa kwa ajili ya ufugaji samaki.
EmoticonEmoticon