Vijana kutoka Arusha maarufu kwa ngoma zao kama kimbaumbau na digidigi wanaojulikana kama Mamongóo (vijana washamba), wamesema kuwa jamii ya sasa hivi inawatisha kutangaza mishe zao wanazofanya nje ya muziki.
Mamong’oo wiki hii wakiwa katika ziara yao kikazi Dar es salaam, wamesema kuwa wao wanajihusisha na biashara nyingi ikiwemo kilimo na ufugaji kama zilivyo jamii nyingi mkoani Arusha. Lakini mtangazaji DJ Tee wa kipindi cha vijana cha Shujaaz alipotaka kufahamu mishe zingine wanazofanya wasanii hao walisema hawawezi kumwaga mchele maana siku hizi wanga ni wengi.
“Sisi pesa zetu hatujahifadhi benki ila tumeziweka sehemu ambayo tunajua zina mzunguko wa kuzalisha, na tumewekeza kwa vijana wenzetu” alisema chalii Jambo kutoka kundi hilo. Hata hivyo, walipoulizwa ikiwa kijana amepata pesa anatakiwa kuwekeza kwenye kitu gani kwanza kati ya shamba, nyumba au ardhi, walisema kwamba ardhi ndio kitu ambacho kinafaa kwa kijana kuwekeza kabla ya kununua gari au hata nyumba maana ardhi inaweza kuleta nyumba na gari.
Wasanii wengi siku hizi wamekuwa na kasumba ya kutumia mishe zao wanazofanya pembeni ya sanaa sio kwa kujiongezea kipato pekee bali kujipatia heshima miongoni mwa fans wao. Mfano mzuri ni msanii Masanja Mkandamizaji ambaye kwa sasa amekuwa akitengeneza mamilioni ya pesa kutokana na biashara ya #KilimoPesa ambapo yeye analima mpunga pamoja na kumiliki mgahawa wa kuuza wali nyama pamoja na biashara zingine tusizozifahamu.
Kipindi cha vijana cha Shujaaz huruka hewani kila Jumamosi saa nne kamili asubuhi kupitia Abood FM ya Morogoro, kisha safari huendelea saa tisa alasiri kupitia East Africa Radio, TBC FM na Chuchu FM ya Zanzibar kwa wakati mmoja, huku KingsFM ya Njombe ikijiunga saa kumi jioni.
EmoticonEmoticon