Mkutano na Waandishi wa habari ukiendelea
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Uganda nchini
Rais
wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni anatarajiwa
kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 25 na 26 Februari
2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mhe.
Rais Museveni anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere tarehe 25 Februari, 2017 majira ya asubuhi na
atapokelewa na Mhe. Dkt Magufuli pamoja na Viongozi wengine wa
Serikali.
Madhumuni
ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uganda na
Tanzania pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya kikanda, kimataifa na
maeneo ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususan katika maeneo ya
Biashara, Nishati, Uchukuzi na yale yanayohusu ujirani mwema.
Wakati
wa ziara hiyo, Mhe. Museveni atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya
faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe
wa pande mbili.
Pia, Mhe. Rais Museveni na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Siku
ya pili, tarehe 26 Februari, 2017, Mhe. Rais Museveni atatembelea
maeneo mbalimbali ikiwemo Viwanda vya Kampuni ya Said Salim Bakhresa
ambaye amewekeza pia nchini Uganda na baadaye Bandari ya Dar es Salaam.
Mahusiano ya Uganda na Tanzania
Mahusiano
ya Tanzania na Uganda ni mazuri na yamekuwa yakiimarika kila mara. Nchi
hizi mbili zimeendelea kushirikiana kwa ukaribu sana katika masuala
mbalimbali ya kiuchumi, kisisasa, kiusalama, kijamii na kikanda hususan
ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia
kumekuwepo ziara za mara kwa mara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi
hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais Uganda, Mhe. Museveni ambaye
alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Mhe. Rais Magufuli zilizofanyika
mwezi Novemba, 2015. Aidha, Rais Magufuli pia alihudhuria sherehe za
kuapishwa kwa Mhe. Rais Museveni mwezi Mei, 2016.
Mahusiano katika Sekta ya Biashara
Mahusiano
ya kibiashara kati ya Tanzania na Uganda yameendelea kuimarika katika
miaka ya hivi karibuni. Katika kipindi cha mwaka 2016 yalikuwa ni mazuri
ambapo Tanzania iliweza kufanya mauzo (exports) ya kiasi cha Shilingi
bilioni 126.744 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 99.882 mwaka 2015.
Mauzo ya Uganda nchini Tanzania (imports) kwa mwaka 2016 yalikuwa ni
Shilingi bilioni 66.849 bilioni ikilinganishwa na Shilingi 78.31 mwaka
2015.
Aidha,
nchi ya Uganda ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania kutokana na jiografia
yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwa nchi jirani tunayopakana
nayo. Uganda ni nchi isiyokuwa na bandari (landlinked country) hivyo
inaitegemea Tanzania kwa ajili ya kupitisha mizigo yake.
Nchi
hiyo imezidi kuwa na umuhimu kufuatia uamuzi wa kupitisha bomba la
mafuta nchini Tanzania, kutoka Kabaale-Hoima, Uganda hadi Bandari ya
Tanga. Bomba hili litakuwa na urefu wa kilomita 1443 na kipenyo cha
inchi 24. Mradi wa ujenzi wa Bomba hili unatarajiwa kukamilika ifikapo
mwaka 2020.
Utekelezaji
wa mradi huu unategemewa kuwa na faida nyingi kwa taifa ikiwemo
kufungua fursa za ajira kwa Watanzania, kuchochea shughuli za kiuchumi
kwa mikoa bomba hilo litakapopita, kufungua ukanda wa biashara wa
kaskazini mwa Tanzania na Uganda na kuimarisha uhusiano katika soko la
Afrika Masahariki.
Ushirikiano kupitia Tume ya pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Uganda
Mkataba
wa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda ulisainiwa Kampala, Uganda
tarehe 13 Machi, 2007. Mkataba huo unaainisha maeneo mbalimbali ya
ushirikiano ambayo yalipaswa kutekelezwa kupitia Tume ya Pamoja ya
Ushirikiano (JPC). Maeneo yaliyoainishwa ni pamoja na Miundombinu,
Viwanda, Biashara, uwekezaji, Nishati, Utalii, Kilimo, Uvuvi, Mazingira,
Ulinzi na Usalama.
Ushirikiano katika jitihada za usuluhishi wa Mgogoro wa Burundi
Jitihada
za usuluhishi wa mgogoro nchini Burundi zinaendelea vizuri. Mhe. Rais
Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa usuluhishi wa mgogoro huo kwa
kushirikiana na Rais Msataafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Benjamin William Mkapa ambaye ni Mwezeshaji wa mazungumzo ya upatanishi
wamekuwa wakifanya jitihada za dhati za kurejesha amani nchini Burundi.
Mhe. Rais Museveni na ujumbe wake wanatarajiwa kuondoka nchini tarehe 26 Februari, 2017.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 23 Februari, 2017
|
EmoticonEmoticon