Mwenyekiti wa Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum.
Mwenyekiti wa Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu baraza hilo kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda za kupambana na wanaojihusisha na dawa za kulevya. Kulia ni Katibu wa Baraza hilo, Padre John Solomon.
Baadhi ya viongozi wa dini (waliokaa), wakiwa kwenye mkutano huo. Wengine ni wanahabari.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale
BARAZA la Viongozi wa dini la kupambana na dawa za kulevya Tanzania ambalo liko chini ya Tume ya kupambana na dawa za kulevya limeunga mkono jitihada zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda za kupambana na watu mbalimbali wanaotumia dawa za kulevya.
Katika hatua nyingine baraza hilo limeiomba serikali kumuongezea ulinzi Makonda kwa kuthubutu kutaja watu wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine na dawa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum ,alisema Makonda anapaswa kuongezewa ulinzi kutokana na ujasiri aliouonesha wa kuthubutu kuwataja kwa majina watu hao.
"Sisi kama baraza tunapinga vita na kulaani hatua yoyote ya kushiriki katika biashra au utimiaji wa dawa za kulevya kwa kuwa matumizi ya dawa hizo yamekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika nchi yetu na yanapotokea nguvu kazi ya Taifa kwa vile wahanga wakubwa wa matumizi ya dawa hizi ni vijana"alisema.
Alisema kutokana na ugumu wa kazi hiyo aliyoianzisha baraza hilo linamuombea kwa mwenyezi mungu ili ampe ulinzi wake na kinga yake na azidi kumpa moyo wa ujasiri wa kupambana na maovu yote yanayo haribu sifa ya Taifa letu na vijana kwa ujumla.
Salum alisema hivi sasa Makonda ameshanza kutengenezewa majungu, fitina na uzushi mbalimbali ili kumkatisha tamaa na aonekane mbaya kwa watanzania lakini hawatafanikiwa endapo atamtanguliza mwenyezi mungu katika mapambano hayo.
Alisema inawezekana wanaopinga au kubeza juhudi hizo ni kwa sababu tu madhara ya dawa za kulevya hayajawagusa wao na familia zao hivyo hawana uchungu na watanzania wenzao walioathirika hivyo wapuuzwe badala yake wasimame pamoja kama watanzania dhidi ya vita hiyo.
Mwenyekiti huyo wa baraza hilo alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wengine waige mfano wa Makonda wa kupambana na uovu huo mkubwa ambao ni janga kwa Taifa kwani Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana.
EmoticonEmoticon