Je, bado unajiuliza ni kwanini mwaka wa 2016 umeisha lakini haujapendezwa na mafanikio uliyoyafikia? Kama ni ndiyo, basi makala haya juu ya kujiwekea malengo itakuwa yenye msaada mkubwa kwako.
Watu wengi bado wanashindwa kuelewa ni kwanini inawawia vigumu kufuatilia hatua za kimaendeleo walizopiga katika maisha yao kutokana na kutojiwekea malengo. Malengo yanatofautiana kulingana na jambo au mambo gani ambayo mtu anatamani kuyatimiza ndani ya kipindi fulani cha muda. Jumia Travel (www.travel.jumia.com) ingependa kukukumbusha haya mapema, kwani bado mwaka 2017 ni mchanga.
Malengo yanaweza kuwa makubwa au madogo, ya muda mrefu au mfupi kutegemea na mtu atakavyojiwekea. Hivyo ni muhimu kutambua kwamba malengo yako ni ya aina gani kwani itakurahisishia namna ya kuyakamilisha. Kwa mfano, lengo la kujenga nyumba ya kuishi haliwezi kufikiwa kwa mbinu au mikakati sawa na kununua samani za ndani.
Hivyo basi katika kujiwekea malengo haitakiwi kujiwekea vikwazo akilini kwamba hauwezi kulifikia lengo fulani kwa sababu ni kubwa, au hauna uwezo wa kulifanikisha. Weka lengo ambalo unaona utaweza kulifikia na kulifanikisha kulingana na uwezo ulionao ndani ya muda uliopo.
Kwa kawaida, maisha ya binadamu yanaongozwa na malengo, hivyo tunaweza kusema kwamba maisha bila ya malengo hayana maana yoyote. Malengo hayo yanaweza kuwa mtu fulani au kupata kitu fulani, inategemea na matamanio ya mtu.
Kuna watu wanatamani kuwa waandishi wazuri wa habari au vitabu na kuwa mfano wa kuigwa lakini hawaonyeshi jitihada zozote za kufikia lengo hilo. Kwa mfano, ili kuwa mwandishi wa habari kwanza kabisa lazima utakuwa umevutiwa na mwandishi mmojawapo katika tasnia hiyo. Je, unafanya jitihada gani za kumfuatilia mtu huyo alipoanza? Changamoto gani alizopitia mpaka akafanikiwa?
Ni ndoto ya kila mwanafunzi kufaulu vizuri shuleni lakini ni wangapi wanafanya bidii ya kufuatilia masomo na kusoma kwa bidii? Wengi wao wanakosa mbinu za kufikia malengo hayo kutokana na kutojiwekea mikakati thabiti, unakuta hahudhurii au kufuatilia vipindi vya darasani wala kujitengea muda wa ziada kujisomea baada ya ule wa darasani.
Hakuna jambo linalowashinda watu wengi kama kujiwekea malengo ya muda mrefu kama vile kutenga fedha kwa ajili ya matumizi ya kitu fulani. Kwa mfano, kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka watu wengi wanalalamika kuwa fedha hakuna huku mahitaji yakiwa ni mengi. Kipindi hiki asilimia kubwa watu wanahitajika kulipia pango za nyumba, karo za shule, leseni za vyombo vya moto na kadhalika. Lakini hayo yote yatasahaulika baada ya mwezi huu kupita pasipo kujiaandaa yasijekutokea tena kipindi kijacho.
Hiyo ni mifano tu ya malengo mtu anaweza kujiwekea, na namna ya kuyafanikisha kwa sababu hiki ndicho kipindi sahihi. Ingawa ni utaratibu mgumu kwa watu wengi hususani Watanzania, ila una faida kubwa sana kama ukiuanza na kuuzingatia.
EmoticonEmoticon