WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza
uongozi Wazara wa Elimu Sayansi na Telnolojia pamoja na Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda mkoani Mtwara
kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha shule tisa za
mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.
Pia ameziagiza halmashauri nchini
kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha wanawasimamia vizuri
walimu jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na hatimaye kupata
matokeo mazuri.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumanne, Januari 17, 2017) wakati akizungumza na watumishi na wananchi
wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo ya Mpanda kwa ajili ya
kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya
Manispaa ya Mpanda.
Kwa mujibu wa matokeo hayo kati ya
shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa
zinatoka katika Mkoa wa Mtwara na moja Tanga. Shule za Mtwara
zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko,
Michiga, Msimbati, Salama na Lukodoka huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.
“Viongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi
na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini
hadi shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani
ya kidato cha pili mwaka jana zitoke huko,” amesisitiza.
Mbali na kuuagiza huongozi wa wizara
hizo kwenda mkoani Mtwara pia Waziri Mkuu amewataka wasimamie vizuri
mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya vizuri na
wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee
kupata matokeo mazuri zaidi.
Awali, akisoma taarifa ya mkoa huo,
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga alisema
katika matokeo ya mtihani kidato cha pili ya mwaka jana mkoa wake
ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa na mkoa wa Geita.
Alisema kwa sasa wanajipanga
kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu wanashika nafasi ya kwanza
kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa Idara ya Elimu, wakuu wa
shule, wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo
yanafanikiwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JANUARI 17, 2017.
EmoticonEmoticon