Wadau kadhaa wa mpira wa miguu, wamemzawadia gari Jonesia Rukyaaa
mwamuzi mwandamizi wa FIFA ambaye hivi karibuni alichezesha vema
michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake iliyofanyika nchini
Cameroon.
Jonesia, ambaye amepata pia kuchezesha mchezo wa watani wa jadi
katika soka nchini miaka miwili iliyopita, alichezesha mechi ya awali na
kuonekana kutokuwa na upungufu kwenye kutafsiri sheria 17 za soka,
alipangwa kuchezesha mechi ya mshindi wa tatu kati ya Ghana na Afrika
Kusini.
Umahiri wake, umevutia wengi wakiwamo wadau wa mpira wa miguu ambao
hawakupenda kutajwa walioamua kumzawadia gari aina Toyota Vits ikiwa ni
zawadi na kumbukumbu yake baada ya kuiwakilisha vema nchi.
Kwa upande wa TFF ilimtuza Mwamuzi Jonesia cheti cha kutambua uwezo
na kufikia hatua ya kulitangaza shirikisho na nchi kwa ujumla. Rais wa
TFF, Jamal Emil Malinzi ndiye aliyemkabidhi funguo za gari Jonasia.
Rais Malinzi alimsifu Jonesia kwa ujasiri na hatua aliyofikia na
kumpa baraka za kumtakia mafanikio zaidi ya hapo ya kusonga mbele baada
ya kufanya vema kwenye michuano ya Afrika Mashariki ya wanawake (CECAFA
challange) na hiyo ya Wanawake Afrika.
“Ni Mtihani mkubwa to officiate (kuchezesha) mechi kubwa kama hiyo.
Maana kila kosa linaweza kukuondoa na mafanikio ya kupata medali ya
dhahabu kati ya waamuzi wanne ni hatua kubwa inayopaswa kutuzwa.
Siwasemi FIFA, lakini itoshe kusema kuwa Jonasia unaweza kufika hatua ya
kuchezesha fainali za kombe la dunia,” alisema Malinzi.
Rais Malinzi alipigia upatu kwa waamuzi wanaume nao kuandaliwa vema
na kuchezesha michezo mikubwa ikiwamo ya fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwani kinachohitajika ni mikakati tu na kuitekeleza.
“Kamati ya waamuzi nawaachia kazi hii. Maana kazi kubwa ya uamuzi ni
kusoma na mazoezi,” alisema Malinzi mbele ya baadhi ya wajumbe wa Kamati
ya Waamuzi akiwamo Mwenyekiti wake, Saloum Chama.
Jonesia ambaye wakati wote alikuwa na faraja, alimshukuru Mungu kwa
mafanikio aliyofikia pia wadau wote wakiwamo wazazi wake na bibi yake
aliyemlea baada ya kufariki mama yake mzazi na viongozi mbalimbali ambao
aliwaelezea kumtia moyo.
EmoticonEmoticon