KLABU
Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa mkoani Kigoma
wikiendi hii Jumamosi (Desemba 3, 2016) kusaka vipaji vya vijana wenye
umri chini ya miaka 17 (U-17).
Huo ni mwendelezo wa mpango wa Kitaifa wa timu hiyo wa kutengeneza
kikosi imara cha timu ya vijana wa umri huo, ambapo inakwenda Kigoma
kutokana na mkoa huo kuwa historia ya kisoka nchini ya kutoa wanasoka
wengi waliotamba.
Majaribio hayo ya pili kuelekea mwisho wa kufungwa zoezi hilo,
yatafanyika ndani ya Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma Jumamosi
hii kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana na vijana wanaotakiwa
ni wale waliozaliwa kuanzia mwaka 2000 hadi 2004.
Mpaka sasa zoezi hilo limeshahusisha mikoa sita, ambayo ni Dar es
Salaam, Tanga, Morogoro & Dodoma, Visiwani Zanzibar, Mbeya na
Mwanza, ambapo kiujumla Azam FC imewafanyia usaili jumla ya vijana 3,
265 na kuvuna 70 pekee kati ya hao waliochaguliwa, huku 151 wakiwekwa
akiba kwenye kumbukumbu za mradi huo.
Vijana hao wote waliochaguliwa kwenye mikoa mbalimbali, wanasubiria
kuitwa kwenye mchujo wa mwisho utakaofanyika ndani ya Uwanja wa Azam
Complex baadaye mwezi huu Desemba, ambao ndio utatoa vijana bora
watakaounda timu hiyo.
EmoticonEmoticon