Kaimu Mkurugenzi Shirika la Maendeleo ya
Petroli Nchini(TPDC) Mhandisi Kapulya Musomba akizungumza na waandishi
wa habari kukanushaTaarifa zinazoenezwa na kampuni ya Dangote pamoja na
washirika wake kupitia mitandao ya Kijamii na vyombo vya Habari kuhusu
kushindwa kukiuzia gesi asilia kwa bei rahisi kiwanda hicho.Kulia kwake
ni Kaimu Kamishana wa Madini Mhandisi John Shija,Kaimu Meneja manunuzi
TPDC Bw.Donal Aponde na Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi.Maria Msellemu.
……………………………..
Na Daudi Manongi-MAELEZO
Kaimu Mkurugenzi Shirika la Maendeleo ya
Petroli Nchini (TPDC) Mhandisi Kapulya Musomba amekanusha taarifa
zinazoenezwa na kampuni ya Dangote kwamba TPDC imeshindwa kukiuzia gesi
asilia kwa bei rahisi kiwanda hicho cha Saruji na hivyo kusababisha
kusimamisha uzalishaji wa kiwanda hicho.
Mhandisi Musomba ameyasema hayo leo Jijini
Dar es Salaam wakati akiongea na waandishi wa habari akitolea ufafanuzi
juu ya suala hilo.
“TPDC imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali
kuhakikisha kwamba kampuni ya Dangote inapata nishati hiyo muhimu kwa
ajili ya kuzalisha saruji ikiwemo kufanyika kwa vikao mbalimbali pamoja
na makubaliano yaliyofanyika kwa Dangote kuridhia nia yao ya kutumia
gesi asilia ili kuzalisha umeme kwa ajili ya kiwanda hicho,”Alisema
Mhandisi Musomba.
Aidha amesema TPDC inafuata kanuni na
utaratibu wa kupanga bei ya gesi asilia ambapo hupanga bei ya gesi
asilia ambapo hupanga kulingana na aina ya wateja waliopo katika makundi
mbalimbali ingawa bei elekezi ambayo inapendekezwa na TPDC lazima
iridhiwe na ipitishwe na EWURA ndipo ianze kutumika.
Vile vile ameeleza kuwa Kiwanda cha
Dangote kimeomba kupewa gesi asilia kwa bei ambayo ni ndogo sana ambacho
ni sawa na kiasi kinachonunulia gesi ghafi kutoka kisimani, na hivyo
haiwezi kuuza gesi asilia kwa bei hiyo kwa sababu kuna gharama
zinazoongezeka katika kuisafisha na kuisafirisha gesi hiyo.
Mhandisi Musomba anasema kuwa wanategemea
ifikapo mwezi Januari 2017 miundombinu ya gesi asilia itakua
imeshaunganishwa na mitambo ya kufua umeme utakaotumiwa na kiwanda
hicho.
Hata hivyo amesema kuwa TPDC inawajali wawekezaji wake akiwemo Dangote ili wawekeze katika kukuza uchumi wa nchi.
EmoticonEmoticon