Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
akihutubia leo mkoani Dodoma katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya
wadadisi wapatao 187 watakaofanya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya
UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 unaotarajia kuanza nchi nzima kuanzia wiki
ijayo. (Picha na Veronica Kazimoto)
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo ya
kina kuhusu Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania katika
hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo unaotarajia kufanyika nchi
nzima kuanzia wiki ijayo. (Picha na Veronica Kazimoto)
Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard
Maboko akizungumza leo mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuhitimisha
mafunzo ya wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI
Tanzania wa mwaka 2016 unaotarajia kufanyika nchi nzima kuanzia wiki
ijayo. (Picha na Veronica Kazimoto)
Mratibu
wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 Bi.
Mariam Kitembe wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu akimkabidhi Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kiasi cha
Shilingi milioni moja na laki sita (1,600,000) zilizochangwa na
wadadisi wa Utafiti huo kwa ajili ya waathirika wa Tetemeko lililotokea
mkoani Kagera hivi karibuni. Mhe. Ummy Mwalimu amekabidhiwa fedha hizo
wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo
mkoani Dodoma. (Picha na Veronica Kazimoto)
Baadhi
ya wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa
mwaka 2016 wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi (hayupo
pichani) wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo
iliyofanyika leo mkoani Dodoma. (Picha na Veronica Kazimoto)
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
(watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Ofisi ya Mtakwimu
Mkuu wa Serikali Zanzibar pamoja na wakufunzi wa Utafiti wa Viashiria na
Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 mara baada ya kufunga mafunzo
ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 leo
mkoani Dodoma. (Picha na Veronica Kazimoto).
………………………………………………………………………………
Na. Emanuel Ghula- Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewaagiza Makatibu
Tawala wa mikoa yote nchini kutoa ruhusa kwa manesi ambao ni wadadisi wa
Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 ili
kufanya utafiti huo.
Akizungumza leo katika hafla ya
kuhitimisha mafunzo ya wadadisi hao iliyofanyika mkoani Dodoma, Waziri
Ummy amesema utafiti huu ni wa muhimu sana hivyo Makatibu Tawala hawana
budi kuwaruhusu manesi hao waliopata mafunzo kufanya utafiti huo.
“Ninawaagiza Makatibu Tawala wote
nchini kuhakikisha wanatoa ruhusa kwa manesi mliopo hapa leo ili muweze
kulisaidia taifa letu kwa kutuletea takwimu sahihi zitakazosaidia katika
kutunga sera na kupanga mipango ya maendeleo hususani katika suala zima
la afya”, ameagiza Mhe. Ummy Mwalimu.
Amefafanua kuwa, takwimu hizi
zitasaidia kuboresha juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali za kusogeza
huduma zinazohusiana na VVU kama vile huduma za upimaji wa VVU bure
katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali, kutoa huduma ya
kupunguza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) pamoja na
utoaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU zijulikanazo kama ARV.
“Utafiti huu ni wa kipekee
ukilinganisha na tafiti zingine zilizofanywa zinazohusu UKIMWI kutokana
na kujumuisha upimaji wa homa ya ini ambao umekuwa tishio katika baadhi
ya nchi barani Afrika”, amesisitiza Mhe. Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa
wananchi wote nchini kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaopita katika
kaya mbalimbali zilizochanguliwa kwa ajili ya kufanya utafiti huu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema utafiti huu
utahusisha watu wote kwenye kaya zipatazo elfu kumi na sita (16,000)
zilizochaguliwa kitaalam na kuwafikia watu wazima wapatao elfu arobaini
(40,000) na watoto zaidi ya elfu nane (8,000).
Dkt. Chuwa ameeleza kuwa, takwimu
hizi zitaisaidia Serikali katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa
sera mbalimbali zinazohusu sekta ya afya nchini hususani upatikanaji wa
huduma za afya.
Wadadisi wapatao 187 ambao ni
manesi kutoka hospitali mbalimbali nchini, wamemaliza mafunzo ya Utafiti
wa viashiria na Matokeo ya UKIMWI ambao unatarajia kuanza wiki ijayo.
Utafiti wa viashiria na Matokeo ya
UKIMWI utahusisha upimaji wa UKIMWI, maambukizi mapya na wingi wa VVU
mwilini kwa watu wanaoishi na VVU, wingi wa chembechembe za kinga
mwilini (CD4 T-cell count), kiwango cha usugu wa dawa za ARV, kiwango
cha maambukizi ya kaswende pamoja na homa ya ini (Hepatitis B na C).