Na Adili Mhina, Dodoma
Tume ya Mipango imehitimisha mafunzo ya Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma yaliyowahusisha maofisa mipango wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri kutoka Mikoa ya Singida, Manyara na Dodoma yaliyofanyika tarehe 12-16 Septemba, 2016 katika ukumbi wa VETA mjini Dodoma.
Akifunga
mafunzo hayo Kaimu Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango, Bibi
Florence Mwanri aliwasihi washiriki kutumia ujuzi waliyoupata katika
kuandaa, kutekeleza miradi ya Umma kwa njia za kisasa ili kuongeza
ufanisi wa miradi na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Alisema
kuwa Tume ya Mipango imefanikiwa kutekeleza wajibu wake wa kuwajengea
uwezo maafisa hao katika hatua zote muhimu zinazopaswa kuzingatiwa
katika kufanya maandalizi, kutekeleza, kusimamia, kufuatilia na kufanya
tahmini ya miradi ya maendeleo.
“Ni
matumaini yangu kuwa hizi siku tano hazijapotea, mmepata elimu ya
kutosha kutoka kwa wataalamu wetu katika masuala yote muhimu yanayohusu
miradi ya Umma. Jukumu mlilonalo kwa sasa ni kuhakikisha mnatumia mbinu
mlizofundishwa katika kutekeleza miradi ya serikali kwa usahihi ili
tufikie malengo ya mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano,”
Alisema.
Nao
washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa wamepata elimu muhimu ambayo
itarahisisha utendaji katika kusimamia miradi na kutoa ushauri wa
kitaalamu katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Walieleza
kuwa mafunzo hayo yamewasisitiza kutumia vigezo muhimu wakati wa
kufanya uchambuzi wa kiuchumi na kifedha ili kufikia uamuzi wa kutambua
miradi ipi ina manufaa na inaweza kupata mikopo katika soko la mitaji.
“vigezo
kama mzunguko wa mradi (project cycle) ikiwa ni pamoja na andiko la
awali (concept note), mchanganuo wa faida na hasara (cost-benefit
analysis) vigezo vya kuchanganua mradi kama vile uwezo wa uzalishaji
(internal rate of return) na thamani halisi ya uwekezaji (Net Present
Value) vimetolewa ufafanuzi mzuri na vimeeleweka na tumevielewa” Alisema
mmoja wa wakufunzi aliyejulikana kwa jina la Jemsi.
Tume
ya mipango inaendelea na zoezi lake la kutoa mafunzo kwa walengwa wakuu
ambao ni wataalam wa Sera na Mipango ambapo kuanzia Septemba 19
wataalamu wa mafunzo hayo watakuwa Mkoani mbeya kwa ajili ya zoezi hilo.
Kaimu
Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (katikati)
akitoa hotuba ya kufunga mafunzo ya Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi
ya Uwekezaji katika Sekta ya Umma kanda ya kati iliyojumuisha mikoa ya
Dodoma, Singida na Manyara katika ukumbi wa VETA mjini Dodoma. Kulia ni
mkufunzi wa mafunzo hayo, dkt. John Mduma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na kushoto ni Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi
Jumla,Tume ya Mipango, dkt. Lorah Madete.
Washiriki wakisikiliza hotuba ya kufunga mafunzo kutoka kwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume Ya Mipango Bibi Florence Mwanri.
Washiriki wanaounda kundi la nne wakijadili maswali juu ya utayarishaji na uchaguzi wa Miradi ya uwekezaji.
Washiriki kundi la kwanza wakijadili maswali waliyopewa na wakufunzi kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo Septemba 16, 2016.
Washiriki kundi la pili wakifanya maswali waliyopewa na wakufunzi mara baada ya kuhitimisha somo.
Washiriki kundi la tatu wakifanya maswali kutoka kwa wakufunzi katika ukumbi wa VETA mjini Dodoma.
EmoticonEmoticon