Shirikisho la Mpira
Miguu Tanzania (TFF) limemteua Sebastian Nkoma kuwa Kocha Mkuu wa timu
ya soka taifa ya wanawake wa Tanzania Bara maarufu kwa jina la
Kilimanjaro Queens ambayo kwa mara ya kwanza inakwenda kushiriki
mashindano ya kuwania Kombe la Afrika Mashariki na Kati yatakayofanyika
kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, 2016 jijini Jinja, Uganda.
Uteuzi huo wa Nkoma unakwenda sambamba na wasaidizi wake, ambao ni
Hilda Masanche na Edna Lema wakati Meneja wa timu hiyo, Furaha Francis.
Mtunza vifaa ni Esther Chabruma maarufu kwa jina la Lunyamila.
Kabla ya uteuzi huo, Nkoma alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Mpira wa
Miguu ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ambayo
kwa sasa ipo kambi ndogo ya kwenye hosteli za TFF kujiandaa na kambi
kubwa itakayofanyika Shelisheli kabla ya kuivaa Congo – Brazzaville
kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa
ya Afrika kwa vijana wenye umri huo. Fainali hizo zitapigwa Aprili
mwakani, nchini Madagascar.
Kilimanjaro Queens inatarajiwa kuanza mazoezi ya leo, Septemba mosi,
2016 ambako wachezaji watakuwa wanakwenda mazoezini Uwanja wa Karume,
Ilala na kurudi nyumbani hadi Jumapili ambako Jumatatu itasafiri kwenda
Uganda kupitia Bukoba mkoani Kagera itakakoweka kambi tena ya siku nne.
Septemba 8, mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi
ambayo pia itakuwa njiani kwenda Uganda kwenye mashindano hayo
yanayoratibiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na
Kati (CECAFA).
Kwa mujibu wa CECAFA, michuano hiyo itafanyika jijini Jinja na
Tanzania ambayo inaongoza kwa ubora wa viwango vya Mpira wa Miguu kwa
nchi za Afrika Mashariki imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za
Rwanda na Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi,
Zanzibar pamoja na mwenyeji Uganda,.
Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12,
2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia
zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa
kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.
Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya
zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar itacheza
na Uganda. Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga
hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.
Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika
Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na
nne.
Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya
kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka
la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania inatarajiwa
kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani
kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa
safari ya Uganda.
EmoticonEmoticon