Na Georgia Misama – MAELEZO
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imejipanga kutoa huduma bora kwa mashirika na taasisi zinazotarajia kuhamia Mjini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano
TTCL Bw. Nicodemus Thom Mushi leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa
akiongea na waandishi wa habari juu ya mpango wa miaka mitatu wa mageuzi
ya kibiashara wa Kampuni hiyo.
Mushi ameeleza kuwa, katika mpango
huo TTCL imejipanga vyema kufanikisha azma ya Serikali ya kuhamia mjini
Dodoma kwa kutoa huduma bora kwani tayari kampuni hiyo ina rasilimali
watu, vifaa na wataalamu wa kutosha katika kutoa huduma za Mawasiliano.
“Nitumie fursa hii kuwaomba
taasisi zote za Umma zinazohamia Dodoma na Taasisi zote kwa ujumla
kutumia huduma za TTCL ambazo zote zimethibitika kuwa ni huduma bora na
za uhakika na zenye gharama nafuu,” amefafanua Mushi.
Aidha, kampuni hiyo imeboresha
njia ya kusikiliza wateja ambapo hivi sasa malalamiko ya wateja
hushughulikiwa ndani ya masaa matatu toka mteja anapotoa taarifa katika
kituo cha huduma kwa mteja.
Akiongelea juu ya maboresho, Mushi
amesema kuwa, kampuni hiyo imeleta huduma mpya ya 4G LET ambayo
inapelekea intaneti yenye kasi zaidi, vile vile imeboresha miundo mbinu
ya mitandao ya simu na data na kuondoa mitambo chakavu.
Sambamba na hayo Mushi
amewahakikishia wateja kuwa TTCL ni kampuni pekee ambayo ni suluhisho la
huduma bora na ya uhakika wakati wote na mahali popote iwe ni nyumbani,
sehemu ya kazi na hata kwenye vyombo vya usafiri kutoka sehemu moja
kwenda nyingine.
EmoticonEmoticon