Baadhi ya viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Limited
uliopo mkoani Katavi, wakimwongoza Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt Medard Kalemani (mwenye Suti ya Bluu-mbele) na Ujumbe wake,
kukagua maeneo mbalimbali ya Mgodi huo wa Kati, akiwa katika ziara ya
kazi mkoani humo hivi karibuni. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Kaimu Mkuu
wa Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian
Matinga.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (mwenye Suti ya
Bluu), akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa wachimbaji wadogo wa
madini katika machimbo yaliyopo wilayani Mlele mkoani Katavi, Salum
Nassoro, alipokuwa katika ziara ya kazi mkoani humo hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (aliyeinama),
akikagua mojawapo ya machimbo ya dhahabu ya wachimbaji wadogo
yaliyopo eneo la Ibindu wilayani Mlele mkoani Katavi hivi karibuni. Wengine
pichani kutoka Kulia ni Mbunge wa Mpanda, Sebastian Kapufi, Kaimu
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Magharibi, Daniel Mapunda,
Msimamizi wa machimbo husika, Mejah Kambaloya, maafisa kutoka
wizarani, Alex Nduye na Mhandisi Yusuph Msembele.
Mmoja wa wamiliki wa Machimbo ya Dhahabu yaliyopo eneo la Kapanda,
wilayani Mlele Mkoa wa Katavi, Peter Gobolo (wa pili kutoka Kulia) akitoa
maelezo kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa
tatu kutoka Kulia) na Ujumbe wake, namna wanavyochenjua Dhahabu kwa
kutumia vifaa vinavyoonekana pichani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (aliyeinua
mkono), akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini waliopo katika
machimbo ya Kapanda wilayani Mlele mkoani Katavi, hivi karibuni
alipokuwa katika ziara ya kazi mkoani humo.
Na Veronica Simba - Katavi
Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuyachukua maeneo ya uchimbaji
madini kutoka kwa wawekezaji wakubwa wasiyoyaendeleza na
kuwapatia watanzania wengine ili wayaendeleze kwa manufaa yao na
ya Taifa kwa ujumla.
Tamko hilo la Serikali lilitolewa kwa nyakati tofauti, hivi karibuni na
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani wakati wa
ziara yake katika Mikoa ya Katavi na Rukwa, kukagua miradi mbalimbali
ya sekta za nishati na madini.
Naibu Waziri alisema kuwa, Serikali imebaini kuna maeneo mengi
ambayo yanakaliwa na watafutaji wakubwa wa madini pasipo
kuyaendeleza hivyo taratibu, sheria na kanuni zitatumika kuyachukua na
kuyagawa kwa wengine.
“Ni kinyume kabisa na kifungu cha 63a, b na c cha sheria ya madini ya
mwaka 2010. Itabidi tuyachukue maeneo hayo ili tuwakabidhi
watanzania wengine wanaoweza kuyaendeleza na tayari tulishaanza
kufanya hivyo.”
Dkt Kalemani alimwagiza Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini,
anayeshughulikia Kanda hiyo ya Magharibi, Daniel Mapunda, kuandaa
orodha mpya ya wawekezaji na watafutaji wa madini ambao wamehodhi
maeneo pasipo kuyaendeleza ili ifanyiwe kazi mapema.
Katika hatua nyingine, akizungumza na viongozi wa Serikali pamoja na
wananchi wa maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Katavi, Naibu Waziri
alibainisha kuwa Mkoa huo ni kati ya mikoa saba inayoongoza kwa
utajiri wa madini nchini na pia ni kati ya mikoa ambayo madini yake
hayajachimbwa ipasavyo.
Alisema, kwa sasa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) wanafanya utafiti
kutambua mbale inayowezwa kuchimbwa kama ni dhahabu au madini
mengine lakini pia wanafanya utafiti wa kijiokemia, kijiofizikia na kijiolojia
ili kujiridhisha kama kuna madini ya kuweza kuchimbwa na wachimbaji
wadogo.
“GST walifanya utafiti huo kwa mara ya mwisho mwezi Aprili mwaka
huu, lakini Serikali tumewataka warudie tena mwishoni mwa mwezi
Agosti ili kabla hatujaanza kuwagawia maeneo ya uchimbaji tuwe na
uhakika.”
Aidha, Dkt Kalemani aliwataka wananchi wanaojishughulisha na
uchimbaji mdogo wa madini kuunda vikundi kwa ajili ya kupata ruzuku
ambayo imetengwa na Serikali. Hata hivyo alisema kuwa, ruzuku hiyo
haitolewi kwa kila mtu isipokuwa wenye vigezo.
Alivitaja vigezo vya msingi kwa mtu kupata ruzuku hiyo kuwa ni pamoja
na muhusika kumiliki leseni ya uchimbaji madini iliyo halali na kwamba
wawe watanzania peke yao pasipo wageni, ambapo alifafanua kuwa
leseni za uchimbaji mdogo ni za watanzania tu kwa mujibu wa kifungu
namba 8 cha sheria ya madini ya mwaka 2010.
Akizungumzia kiwango cha fedha za ruzuku ambacho Serikali imetenga
kwa mwaka huu, Dkt Kalemani alisema kuwa ni shilingi bilioni 6.68.
EmoticonEmoticon